Putin: 'Ni upuuzi tu' kudai kwamba Russia inapanga kuishambulia kijeshi NATO
(last modified Thu, 28 Mar 2024 10:08:07 GMT )
Mar 28, 2024 10:08 UTC
  • Putin: 'Ni upuuzi tu' kudai kwamba Russia inapanga kuishambulia kijeshi NATO

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, nchi yake haina nia ya kuingia kwenye makabiliano ya kijeshi na vibaraka wa Marekani wa Ulaya Mashariki.

Putin ameyasema hayo alipotembelea kituo cha jeshi la anga cha Torzhok kilichoko kwenye mkoa wa Tver.

Rais wa Russia ametangaza msimamo huo kufuatia matamshi ya maafisa kadhaa wa nchi za Magharibi ambao wamehimiza na kupigia upatu suala la kutolewa msaada wa ziada wa kijeshi kwa Ukraine kwa madai kuwa Moscow haitakoma kuendeleza hujuma za kijeshi ikiwa Kiev itashindwa kwenye uwanja wa vita.

"Huu ni upuuzi tu," amesema Putin, akibainisha tofauti iliyopo katika matumizi ya kiulinzi ya Russia ikilinganishwa na bajeti za kijeshi za NATO; na akaongezea kwa kusema: "madai kwamba tutashambulia Ulaya baada ya Ukraine ni upuuzi mtupu na vitisho wanavyotoa kwa watu wao wenyewe ili tu wawakamue fedha".

Rais Putin wa Russia (kushoto) na Rais Biden wa Marekani

Rais wa Russia amefafanua kwa kusema, satelaiti za Marekani zilizoko Ulaya Mashariki hazina sababu ya kuogopa, kwa sababu mazungumzo juu ya uwezekano wa kufanywa shambulio na Russia dhidi ya Poland, Jamhuri ya Czech au nchi za Baltic ni propaganda tu za serikali zinazojaribu kuwatisha raia wao ili kuchukua kutoka kwao gharama za ziada kwa kuwafanya wabebe mzigo huo mabegani mwao.

Katika hotuba yake hiyo, Putin ameendelea kueleza kwamba, ni NATO ndiyo imekuwa ikijipanua kuelekea mipaka ya Russia, si vinginevyo; na kwamba inachofanya Moscow ni kulinda watu wake tu kwenye maeneo ya ardhi yake ya kihistoria.

Rais wa Russia amesma: "walikuja mpaka kwenye mipaka yetu… Je, sisi tulivuka bahari kwenda hadi kwenye mipaka ya Marekani? Hapana, wanatukaribia, na wamekaribia sana”.../