Apr 18, 2024 04:33 UTC
  • Wabunge Uingereza waitaka serikali isitishe kuiuzia silaha Israel

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza imepokea waraka wa maombi wenye jumla ya saini lfu 70 zikiwemo saini za baadhi ya wawakilishi wa Bunge la nchi hiyo wanaotaka kusitishwa kutumwa mabomu na makombora ya nchi hiyo kwa Israel.

Tovuti ya Muungano kwa jina la Palestine Solidarity Campaign yaani Kampeni kwa ajili ya Mshikamano na Palestina ya nchini Uingereza imetangaza katika taarifa yake na kuchapisha picha za baadhi ya wabunge wa nchi hiyo waliohudhuria hafla iliyofanyika jana huko London kwamba zaidi ya mawakili elfu moja, maprofesa wa kitivo cha sheria wa Vyuo Vikuu na majaji wastaafu nchini Uingereza wameandika katika waraka wao kwamba hatua ya serikali ya London ya kuitumia Israel mabomu na makombora ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. 

Hapo awali, wabunge 135 wa Bunge la Uingereza, katika barua iliyotumwa kwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni na wa Biashara wa nchi hiyo wameitaka serikali ya nchi hiyo isitishe uuzaji wa silaha kwa Israel. 

Imeeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za serikali ya Uingereza; serikali ya London haiwezi kuiuzia silaha na zana za kijeshi nchi ambayo inakiuka sheria za kimataifa.  

Taarifa ya Muungano wa Kampeni kwa ajili ya Mshikamano na Palestina wa nchini Uingereza imeeleza kuwa Canada, Uholanzi, Japan, Uhispania na Ubelgiji zimetangaza kusitisha kuiuzia silaha Israel, hata hivyo  David Cameron Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, amesema wataendelea kuiuzia silaha Israel.  

David Cameron 

Taarifa ya Palestine Solidarity Campaign imeendelea kubainisha kuwa: Mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina, mashambulizi dhidi ya Lebanon, Syria na Iran yanadhihirisha namna Uingereza inavyoendelea kuiuzia Israel mabomu na makombora; hatua inayoipelekea London kuwa mshirika wa utawala wa Kizayuni katika kukiuka sheria za kimataifa na katika maafa ya vita vinavyojiri katika eneo. 

Tags