Apr 19, 2024 02:45 UTC
  • New York Times: Israel haikutarajia kabisa kupata majibu makali kama yale kutoka kwa Iran

Gazeti la New York Times la nchini Marekani limefichua kuwa, ushahidi uliopatikana kutoka kwenye duru za ndani za Israel unathibitisha kuwa Tel Aviv haikutarajia kabisa kupata majibu makali kiasi chote kile kutoka kwa Iran baada ya kuushambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus Syria.

Shirika la habari la FARS limelinukuu gazeti hilo maarufu la nchini Marekani likiandika: "Waisraeli walikosea mno katika mahesabu yao na kamwe hawakufikiria kuwa Iran itatoa majibu makali."

Gazeti hilo limeandika ripoti yake hiyo kwa kunukuu maneno ya maafisa kadhaa wa Marekani ambao walishiriki kwenye vikao vya ngazi za juu vya kujadili hali iliyojitokeza baada ya Iran kuutia adabu utawala wa Kizayuni. Vikao hivyo vilihusisha pia maafisa na viongozi wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni.

Makombora ya Iran

 

Katika toleo lake la jana Alkhamisi, gazeti la New York Times limesema kuwa, viongozi wa Marekani walikasirika baada ya kudharauliwa na viongozi wa Israel ambao hawakuwapa taarifa kuhusu nia yao ya kushambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus isipokuwa katika dakika za mwisho za kabla ya kufanyika shambulio hilo.

Katika ripoti yake hiyo, gazeti la New York Times limefichua kwamba, katika nyaraka za siri za ndani ya Israel zilizozungumzia uwezekano wa Tehran kujibu mashambulio hayo, hakuna hata sehemu moja iliyoweka uwezekano wa Iran kujibu shambulizi hilo kwa kutumia ndege 300 zisizo na rubani. 

Gazeti hilo la Marekani pia limeandika: Tangu mwanzo Israel ilikuwa inatarajia kwamba kama Iran ingejibu mashambulizi basi ingetumia makombora kama 10 ya ardhi kwa ardhi na katika kipindi cha wiki moja kabla ya shambulio ya Iran, Israel ilikuwa imetabiri kuwa huenda Jamhuri ya Kiislamu ingelitumia makombora 60 hadi 70 ya ardhi kwa ardhi, lakini hali ilikuwa kinyume kabisa na matarajio ya Israel.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo imesema kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa Marekani wameliambia gazeti la New York Times kuwa, tarehe 3 Aprili, waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin alizungumza na waziri wa vita wa Israel na kumlalamikia kwamba utawala wa Kizayuni umeshambulia ubalozi wa Iran bila ya kuitaarifu Washington na hivyo kuwaweka kwenye hatari wanajeshi wa Marekani na hata haikuwapa indhari ya mapema la kuweza kujiweka sehemu salama.