Apr 20, 2024 12:17 UTC
  • Marekani; kizuizi kikuu kwa Palestina kuwa mwanachama kamili katika Umoja wa Mataifa

Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa Israel kwa mara nyingine imetumia kura ya turufu (Veto) na kuzuia kupasishwa uanachama kamili wa Palestina ndani ya Umoja wa Mataifa.

Katika kikao kilichofanyika kuhusu suala hilo, kati ya wajumbe 15 wa Baraza la Usalama, wajumbe 12 walipiga kura kuunga mkono azimio hilo kuhusu Palestina huku Uingereza na Uswisi zikijizuia na Marekani ikalipiga veto azimio hilo kwa kura ya hapana.   

Suala la kuipa uanachama Palestina katika Umoja wa Mataifa ni jinamizi kwa Tel Aviv na kwa msingi huo utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu Marekani zimekuwa zikipinga vikali Palestina kupewa unachama kamili katika UN. Ni wazi kuwa kutekelezwa suala hilo inaweza kuwa hatua kubwa kwa ajili ya kufanikisha uundaji wa nchi huru ya Palestina, suala ambalo linahesabiwa kuwa sawa na kipigo kikali kwa utawala wa Kizayuni kwa kuzingatia kuingia madarakani moja ya serikali yenye misimamo mikali zaidi ya utawala huo haramu.   

Gilad Erdan, Mwakilishi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa, kwa kuhofia kufikiwa suala hilo amedai kuwa juhudi za Palestina kuwa mwanachama wa kudumu wa Umoja wa Mataifa zitafeli na Israel itatumia mbinu yoyote ile kusambaratisha jambo hilo, na kwamba Marekani na wanachama wengine wa Baraza la Usalama pia wanapinga Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umojaj wa Mataifa.  

Gilad Erdan

Palestina hivi sasa ni mwangalizi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa; na mwaka 2011 iliomba uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo, mwezi wa Aprili, Palestina pia iliomba kupitia barua iliyoituma kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba suala la kujiunga kwake na Umoja wa Mataifa kama mwanachama wa kudumu linapasa kuchunguzwa kwa mara nyingine tena. 

Kwa mujibu wa sheria za sasa iwapo nchi 9 kati ya wanachama 15 wa Umoja wa Mataifa watapiga kura ya ndio kuunga mkono ombi la nchi moja kuwa mwanachama wa UN; Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litapasa kuchunguza suala hilo lakini iwapo tu hakutakuwa na nchi yoyote mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama yaani Uingereza, China, Russia, Marekani na Ufaransa itakayolipinga ombi hilo. 

Kutambuliwa taifa la Palestina kwa kutilia maanani vita vya Gaza na jinai kubwa za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na vilevile  fikra za waliowengi na nchi mbalimbali duniani kulaani vikali jinai hizo, ni pigo kwa utawala wa Kizayuni. Kwa msingi huo, Marekani ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa utawala huo kwa mara nyingine tena imefunga njia ya kufikiwa jambo hilo kwa kulipiga veto ombi la Palestina. 

Washington imetekeleza hatua hiyo katika hali ambayo Marekani siku zote imekuwa ikizungumzia kuundwa nchi mbili ili kuupatia ufumbuzi mzozo kati ya Palestina na Israel hata hivyo kivitendo Marekani ndiyo inayokwamisha kutambuliwa rasmi haki za Wapalestina zisizokanushika. 

Mwakilishi wa Marekani UN, Linda Thomas Greenfield ambaye nchi yake ilipiga kura ya turufu dhidi ya Palestina

Marekani inaashiria mazungumzo hayo huku ikiuunga mkono kwa hali na mali utawala wa Kizayuni, kwa kuupatia silaha na kuudhaminia bajeti ya kijeshi, huku ikizuia kupasishwam sheria yoyote dhidi ya Uzayuni katika taasisi za kimataifa na hivyo kuwa mshirika wa Israel katika jinai dhidi ya Wapalestina, na nchi inayohami maslahi haramu ya Tel Aviv. Kwa hakika, hatua ya Marekani ya kulipigia kura ya turufu ombi lolote kuhusu haki za Wapalestina inauandalia uwanja utawala wa Kizayuni wa kuendeleza mashambulizi dhidi ya Gaza, mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kuharibu kikamilifu  miundombinu ya eneo hilo. 

Mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza 

Hivi sasa pia licha ya jamii ya kimataifa kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina; kwa mara nyingine tena huku ikidai kutetea haki za binadamu imewafungia njia Wapalestina na kuuhami utawala wa Kizayuni ili uendeleze jinai zake dhidi ya wakazi wa Gaza, bila kujali matakwa na maombi ya kimataifa. 

 

 

Tags