Erdogan: Netanyahu, mwenye kiu ya damu sharti akomeshwe
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwa mara nyingine amemshambulia vikali kwa maneno Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu na kumtaja kama mtu mwenye kiu ya kumwaga na kufyonza damu.
Akihutubia mkutano wa chama tawala cha Haki na Ustawi katika mji wa Ankara, Erdgogan ameashiria jinai zinazofanywa na Netanyahu katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, dunia inapasa kumdhibiti mwanasiasa huyo mwenye kiu ya damu, na ambaye amelisambaratisha eneo.
Erdogan ameeleza bayana kuwa, Uturuki itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha kuwa dunia inaitambua Israel kama dola la kigaidi, huku akiwataja wanamuqawama wa Palestina kama wapigania ukombozi wa taifa lao.
Kadhalika Rais wa Uturuki ametoa mwito kwa mataifa ya Waislamu kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kukomesha jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Huko nyuma pia, Erdogan alisema Netanyahu amempiku kiongozi wa Wanazi Adolf Hitler kwa kuua makumi ya maelfu ya watoto wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Licha ya Rais Erdogan wa Uturuki kusikika mara kadhaa majukwaani akitoa hotuba kali za kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, lakini serikali yake imekuwa ikilaumiwa na kukosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa kuendelea kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na utawala huo katili.