Wizara: Watoto wanabakwa katika kambi za wahajiri Marekani
(last modified Sat, 20 Jul 2024 06:10:34 GMT )
Jul 20, 2024 06:10 UTC
  • Wizara: Watoto wanabakwa katika kambi za wahajiri Marekani

Imebainika kuwa, maelfu ya watoto wahajiri wamebakwa na kufanyiwa unyanyasaji na udhalilishaji wa kingono katika kambi na vituo vya 'kuwahifadhi' wahamiaji haramu nchini Marekani.

Wizara ya Sheria ya Marekani imefichua katika faili ililoliwasilsha mahakamani kuwa, katika muda wa miaka 8 iliyopita, maelfu ya watoto wadogo wamelawitiwa, kubakwa na kunyanyaswa kingono katika vituo wanavyowekwa wahajiri.

Kwa mujibu wizara hiyo, kesi hizo za ubakaji, unyanyasaji na udhalilishaji huo wa kingono dhidi watoto wadogo zimefanyika baina ya mwaka 2015 na 2023 katika kambi za wahajiri zinazosimamiwa na shirika la Southwest Key, hasa katika majimbo ya Texas, Arizona, na California.

Habari zaidi zinasema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, mamia ya wahajiri wamefanyiwa udhalilishaji wa kingono nchini Marekani na maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha wa nchi hiyo.

Mamilioni ya wahajiri wanaingia Marekani kila mwaka kwa kutumia 'njia za panya' hasa kwenye mpaka mrefu wa Marekani na Mexico. Idadi ya wahajiri wanaoingia Marekani kimagendo imevunja rekodi wakati wa urais wa Joe Biden.

Takwimu za Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani zinaonesha kuwa, wahajiri milioni 8.2 wakiwemo watoto wadogo wamewasili Marekani kupitia mipaka ya kusini tangu Biden aingie madarakani Januari 2021, ikilinganishwa na wahamiaji milioni 5.5 wakati wa uongozi wa watangulizi wake, Barack Obama na Donald Trump.

 

Tags