Assad: Huenda Erdogan atatumia 'mapinduzi' kuwaondoa maadui serikalini
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema huenda Rais Reccep Teyyip Erdogan wa Uturuki akatumia jaribio la mapinduzi yaliyofeli kuwaadhibu na kuwaondoa serikalini wakosoaji na wapinzani wake.
Rais Assad amenukuliwa akiyasema hayo na gazeti la Al-Akhbar la Lebanon ambalo limeandika habari kuhusu mkutano kati yake na ujumbe wa wanasiasa wa Lebanon unaoongozwa na Najah Wakim, kiongozi wa Harakati ya Wananchi ya Lebanon mjini Damascus. Rais wa Syria amesema jaribio la mapinduzi ya kijeshi na matukio ya hivi sasa nchini Uturuki yamezungukwa na utata na siri kubwa na kusisitiza kuwa, huenda Rais Erdogan akayatumia matukio hayo kuwaondoa wapinzani wake kwenye taasisi za serikali kama mahakama na jeshi la nchi hiyo. Tayari maelfu ya wanajeshi wanaodaiwa kuhusika na mapinduzi hayo wametiwa nguvuni huku maelfu ya majaji wakipigwa kalamu nyekundu. Rais Erdogan alijitokeza mapema Jumamosi katika televisheni ya taifa na kusema mapinduzi yamefeli na kwamba waliotekeleza jaribio hilo la mapinduzi ni wahaini na watachukiliwa hatua. Watu zaidi ya 250 waliuawa katika jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi lililogonga mwamba.