Juhudi za wajumbe wa Kiislamu katika Kongamano la Kitaifa la Democratic kwa ajili ya kuiwekea vikwazo Israel
Makumi ya wajumbe na makundi ya Kiislamu yanayokerwa na uungaji mkono wa Marekani kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, wanapanga kufanya mabadiliko katika mpango wa uchaguzi wa Chama cha Democratic na kutilia mkazo suala la kuwekwa vikwazo vya silaha dhidi ya Israel.
Kongamano hilo la siku nne lilianza jana Jumatatu mjini Chicago, na Kamala Harris anatazamiwa kutangazwa rasmi kuwa mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Marekani baadaye mwaka huu.
Kundi la watetezi wa Palestina wanaojiita "Wajumbe Dhidi ya Mauaji ya Kimbari" linasema litatumia haki yake ya uhuru wa kujieleza katika Kongamano la Kitaifa la Chama cha Democratic wiki hii kutoa hoja na matakwa yake. Kundi hilo linataka kupigwa marufuku msaada wa silaha kwa watu na makundi ambayo yamekiuka haki za binadamu. Liano Sharon, mwanachama wa kundi hili, amesema: "Tunataka sauti yetu isikike." Brandon Johnson, meya wa Chicago, amesema katika mkesha wa Kongamano la Kitaifa la chama cha Democratic linalofanyika katika mji huo, kwamba vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza ni mauaji ya kimbari.
Rasimu ya ilani ya chama cha Democratic iliyotolewa katikati ya mwezi Julai, inataka "kusitishwa mara moja na daima mapigano" huko Gaza na kuachiliwa huru mateka. Hata hivyo, rasimu hiyo haikugusia kabisa raia zaidi ya 40,000 wa Gaza, ambao wengi wao ni watoto na wanawake, waliouawa shahidi katika vita vya Israel, na pia haijazungumzia haja ya kuwekwa kikomo kwa misaada ya silaha ya Marekani kwa Israel. Hii ni licha ya ukweli kwamba, wiki jana Marekani iliidhinisha msaada mwingine wa silaha wenye thamani ya dola bilioni 20 kwa Israel.
Licha ya himaya na msaada mkubwa wa kisiasa na kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na licha ya utawala huo kukaidi matakwa ya jamii ya kimataifa ya kusimamisha vita vya Gaza, utawala wa Joe Biden unatosheka kutoa maonyo yasiyo na taathira yoyote kwa Tel Aviv bila kutumia mashinikizo ya kisiasa na kifedha kuilazimisha Israeli isitishe vita vya Gaza. Vilevile, wakati utawala wa Kizayuni ukiendelea kufanya mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza na kutumia silaha ya njaa kuwatesa Wapalestina, serikali ya Biden inatumia ushawishi wake kuzuia harakati yotote ya kulaaniwa utawala huo katika taasisi za kimataifa na pia kushughulikia uhalifu huo kwenye mahakama za kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
Inatupasa kusisitiza hapa kuwa, utawala wa Biden unatekeleza sera za kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na Israel. Wakati idadi kubwa ya wabunge wa chama cha Democratic katika Kongresi ya Marekani wakipinga kuuziwa silaha utawala wa Kizayuni, Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, inaendelea kuipatia silaha Tel Aviv na kupeleka shehena kubwa ya zana za kijeshi na mabomu yenye nguvu kwa utawala wa Kizayuni ili kuwaua wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza. Ni wazi kwamba, misaada hii isiyo na mpaka ya Ikulu ya White House kwa Tel Aviv imekuwa mwanga wa kijani kwa Israel wa kuendeleza mauaji ya kimbari huko Palestina na kutumia silaha ya njaa kuangamiza kizazi cha wakazi wa Gaza. La kusikitisha zidi ni kuwa, sambamba na haya yote, White House inadai kwamba inataka kusitishwa vita vya umwagaji damu huko Gaza!
Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, kama kweli Joe Biden anataka kusitishwa vita Gaza, kwa nini haweki mashinikizo yoyote kwa Israel, au kwa uchache kkwa nini hachukui hatua ya kusitisha utumaji wa mabomu kwa utawala wa Kizayuni ambayo yanawalenga moja kwa moja watu wa Gaza?
Sera hizi za kinafiki za serikali ya Joe Biden kuhusu vita vya Gaza na kuendeleza himaya na misaada ya kijeshi na silaha kwa utawala wa Kizayuni vimekuwa sababu ya kupungua uungaji mkono wa wapiga kura Waislamu na Waarabu wa Marekani kwa Chama cha Democratic.