Kuongezeka dhulma na vitendo vya mabavu dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani
Mwenendo wa chuki na unyanyasaji dhidi ya Uislamu na Waislamu umeongezeka sana katika nchi za Ulaya hususan Ujerumani, kiasi kwamba takwimu rasmi zinaonyesha kuwa hali ya kijamii nchini humo inazidi kubana na kuwakandamiza Waislamu.
Gazeti la De Welt limeandika kuhusu suala hili kwamba, kwa mujibu wa ripoti ya polisi ya Ujerumani, katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kesi 42 za majeraha ziliripotiwa kutokana na uhalifu uliofanywa kwa nia ya chuki dhidi ya Uislamu.
Katika miaka ya hivi karibuni, chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, vituo vya kidini na mikusanyiko yao zimekuwa zikizingatiwa kuwa miongoni mwa siasa za serikali za Ulaya za kuuweka Uislamu na Waislamu katika mashinikizo na mateso kwa visingizio mbalimbali visivyo na msingi.
Wakati huo huo, Waislamu wa Ujerumani na Ufaransa wana hali ngumu zaidi kuhusu suala hilo. Nchi hizi mbili zilizo na idadi kubwa zaidi ya Waislamu, zimeongeza moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja mashinikizo na vitendo vya ukatili dhidi ya Waislamu katika miaka ya hivi karibuni, hususan katika miezi ya karibuni. Kwa mujibu wa matokeo ya hivi karibuni ya utafiti wa Shirika la Haki za Msingi la Ulaya (FRA), Waislamu nchini Ujerumani wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa zaidi wa rangi barani Ulaya baada ya Austria.
Nchini Ujerumani, suala la chuki dhidi ya Uislamu limekuwa tatizo kubwa kwa Waislamu. Petra Pau, mwakilishi wa chama cha mrengo wa kushoto katika Bunge la Ujerumani, amesema, akiashiria takwimu alizopewa na serikali kwamba ripoti hizo zinatia wasiwasi mkubwa na kuwa mashambulizi yamezidi kuwa ya kikatili. Akizungumzia kuongezeka kwa idadi ya wahanga wa ukatili unaosababishwa na chuki dhidi ya Uislamu, Pau amesema: 'Hali inaonyesha ni kwa kiwango gani tishio hili lilivyo kubwa kwa watu wanaochukuliwa kuwa Waislamu na jinsi hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kuwalinda na kuzuia uhalifu dhidi yao".
Waislamu nchini Ujerumani wamekabiliwa na mashinikizo na ghasia zaidi katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kutokana na kuendelea kwa vita vya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Serikali ya sasa ya Ujerumani ambayo ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa utawala haramu wa Israel sio tu inaisaidia Israel kifedha na kwa silaha katika vita vya Gaza tangu kuanza vita katika eneo hilo, bali pia inawatambulisha Waislamu kuwa waungaji mkono wa Wapalestina na hivyo kuchochea hisia za chuki dhidi yao kutoka kwa watu na makundi yenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Waislamu.
Robert Habeck, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani amezituhumu baadhi ya jumuiya za Kiislamu nchini Ujerumani kwa kusitasita kutangaza kujitenga kwao na Hamas au kupinga kile kinachodaiwa kuwa ni chuki dhidi ya Mayahudi. Habeck amesisitiza kwamba Waislamu wanaoishi Ujerumani lazima watangaze waziwazi kujitenga kwao na chuki dhidi ya Mayahudi, vinginevyo watapoteza haki ya kutendewa haki na kutobaguliwa. Serikali ya Ujerumani imetayarisha mazingira ya kushambuliwa na kunadamizwa Waislamu na makundi yenye itikadi kali za chuki nchini humo, katika hali ambayo kisiasa katika miezi ya hivi karibuni, vyama na makundi ya mrengo wa kulia ambayo yana siasa za chuki dhidi ya Waislamu na wahajiri yamepata ushindi mkubwa katika medani ya siasa ya nchi hiyo.
Vyama vya mrengo wa kulia daima vimekuwa vikikosoa uwepo wa Waislamu katika nchi hiyo na vimekuwa na misimamo mikali dhidi yao, kiasi kwamba Ayman Mazik, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini humo ameonyesha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka idadi na ushawishi wao nchini na kuonya: 'Hali hii ni tishio kwa demokrasia nzima.'
Farda Ataman, Kamishna wa Shirikisho la Kupambana na Ubaguzi la Ujerumani, pia ametahadharisha kuhusiana na suala hilo na kusisitiza kwa kusema: 'Uadui dhidi ya Waislamu umefikia kiwango ambacho kinapasa kupingwa na kukabiliwa."
Mashinikizo dhidi ya Waislamu na Uislamu hayafanyiki tu nchini Ujerumani bali pia katika nchi nyingine nyingi za Ulaya. Huko Ufaransa, licha ya madai yote ya serikali ya nchi hiyo kuzingatia uhuru, Waislamu wanakabiliwa na matatizo makubwa ambapo hata hawaruhusiwi kuvaa hijabu na wanawake wa Kiislamu wamepigwa marufuku kujisitiri kwa vazi la burqa. Kuchomwa moto msikiti wa Waislamu katika mji wa Amiens, makao makuu ya eneo la Picardy kaskazini mwa Ufaransa, katika kipindi cha wiki moja iliyopita ni mfano mwingine wa wazi wa kuongezeka mashinikizo na vitendo vya mabavu dhidi ya Waislamu. Waislamu wanakabiliwa na hali ngumu pia katika nchi nyingine za Ulaya.
Kwa hakika, mambo kama vile upinzani wa Waislamu dhidi ya vita vya Gaza na kuuawa kinyama Wapalestina, propaganda za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi za kuwafanya Waislamu waonekane kama ni magaidi, utekelezaji wa siasa za unyanyasaji katika nchi nyingi za Ulaya dhidi ya jamii za walio wachache na wahajiri, ni baadhi ya mambo ambayo yamefanya hali ya Waislamu wanaoishi katika nchi hizo, na hasa Ujerumani kuwa ngumu zaidi.