Kulaaniwa na Jumuiya ya NAM uvamizi wa Israel dhidi ya Iran
Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), imelaani uovu wa utawala wa Kizayuni na hujuma yake ya makusudi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutangaza kuwa, shambulio hilo ni ukiukaji mkubwa wa mamlaka na umoja wa ardhi ya Iran.
Katika taarifa yake juzi Jumatatu, Jumuiya ya NAM imelaani kwa nguvu zote kitendo cha Israel cha uchokozi wa makusudi, ambacho kinahesabiwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa mamlaka na ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupelekea kuuawa shahidi askari wanne wa jeshi la anga la Iran na raia mmoja.
Iimeelezwa bayana katika taarifa ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kwamba: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yamekiuka misingi mikuu ya sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, hususan kifungu cha 2, kipengee cha 4, ambacho kinakataza kwa uwazi matumizi ya nguvu dhidi ya mamlaka na umoja wa ardhi wa nchi yoyote.
Kuhusiana na hilo, Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, huku ikiibebesha Israel jukumu la uvamizi huo na matokeo yake, ambayo yanahesabiwa kuwa tishio kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa, haki ya asili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine zilizoathirika inathiibitishwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa na hati ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa ya kulinda mamlaka, umoja wa ardhi yake na usalama wa watu wake.
Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote pia imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake kwa kulaani waziwazi kitendo hicho cha uchokozi na kuchukua hatua zinazostahiki ili kuzuia kukaririwa vitendo kama hivyo.
Msimamo madhubuti na wa wazi wa Jumuiya ya NAM katika kulaani hujuma ya Israel dhidi ya Iran kufuatia operesheni ya makombora ya Ahadi ya Kweli-2 ya Iran unaweza kuonekana kuwa ni mfano mwingine wa kuzidi kutengwa utawala wa Kizayuni na vilevile kupatikana makubaliano ya kimataifa dhidi ya vitendo vya kihalifu vya utawala huo ghasibu.
Umuhimu wa taarifa ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) katika suala hili kimsingi unatokana na idadi kubwa ya nchi wanachama wa vuguvugu hilo na katika hatua inayofuata, msimamo wa pamoja wa nchi hizi katika kulaani kitendo cha Israel.
Kambi ya Magharibi ikiongozwa na Marekani, imechukua msimamo wa pamoja wa kuiunga mkono Israel tangu kuanza kwa vita vya Gaza kufuatia operesheni ya kimbunga ya Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba, 2023. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita madola ya Magharibi na hasa Marekani imetuma mafuriko ya silaha na zana za kivita kwa Israel kwa ajili ya mauaji ya halaiki ya Wapalestina.
Wakati huo huo, Marekani ikiwa mshirika wa kimkakati wa Israel, imekuwa ikiuunga mkono utawala huo kisiasa kwa maazimio ya kura ya turufu.
Wakati wa shambulio la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Marekani ilitoa baraka za kufanyika shambulio hilo. Marekani ilitoa msaada wa vifaa kwa shambulio hili kwa kutoa taarifa na kutuma ndege za kujaza mafuta, na anga ya Iraq pia ilikuwa katika udhibiti wa ndege za kivita za utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuishambulia Iran.
Wamagharibii kwa ujumla isipokuwa nchi chache kama vile Uswisi, hawakuchukua misimamo dhidi ya mashambulizi ya utawala huo ghasibu na kimsingi waliunga mkono shambulio hilo kwa njia isiyo wazi. Baadhi ya nchi za Magharibi zilitoa taarifa inayozitaka pande zote mbili zijizuie, yaani Iran na Wazayuni.
Hii ni pamoja na kuwa nchi nyingi za Asia Magharibi na sehemu nyingine za dunia zililaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran kwa kauli tofauti.
Hii inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya dunia inafahamu tabia ya Israel ya uchokozi na kupenda vita na nafasi yake hasi katika kuleta hali ya wasiwasi, ukosefu wa utulivu na vita katika eneo hili.
Kwa njia hiyo ni lazima kusema kuwa, nguvu laini ya utawala wa Kizayuni imekabiliwa na mmomonyoko unaozidi kuongezeka, na licha ya juhudi za Washington za kutoa sura nzuri na ya haki ya utawala huo na kuutambulisha kuwa ndio demokrasia pekee katika Mashariki ya Kati, lakini taswira ya walimwengu kwa Israel ni mvamizi na mpenda vita.