Jul 24, 2016 04:30 UTC
  • Zarif: Masunni na Mashia lazima waungane kuzima ugaidi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani hujuma ya kigaidi ya hapo jana iliyosababisha vifo vya makumi ya watu nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa, wakati umefika kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni waungane kwa shabaha ya kulikabili kwa pamoja jinamizi la ugaidi.

Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa twitter, Mohammed Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema shambulio hilo la jana katika mji wa Kabul nchini Afghanistan na taathira zake hasi ni mfano hai wa kuonyesha namna ugaidi hauchagui dini wala madhehebu na kusisitizia haja ya Waislamu kushikamana ili kung'oa mizizi ya ugaidi kwa pamoja.

Athari za mashambulizi ya Kabul, Afghanistan

 

Waislamu 83 waliuawa na wengine zaidi ya 260 kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh dhidi ya maandamano ya amani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Shambulizi hilo lilifanyika katika eneo la Deh Mazang mjini Kabul ambako maelfu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliandamana kwa amani kulalamikia mradi wa umeme uliozusha mjadala mkubwa. Wakati huohuo, Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amelaani hujuma hiyo ya kigaidi ya Kabul na kusema kuwa, ugaidi na misimamo ya kuchupa mipakani ni mambo ambayo yanatishia usalama na maisha ya watu wasio na hatia na kuongeza kuwa, jinamizi la ugaidi haliwezi kuzimwa pasina umoja na ushirikiano wa nchi za dunia.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan akisisitiza jambo

 

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan kadhalika amelaani mauaji hayo na kusema, amesikitishwa mno na shambilizi hilo na kuashiria kuwa, ni haki ya kila raia kuandamana kwa amani na kwamba magaidi wametumia fursa hiyo kulipua mabomu yaliyoua wananchi wakiwemo maafisa wa usalama na ulinzi. 

Tags