Jul 26, 2016 16:49 UTC
  • Hollande: Tutatumia kila njia kukabiliana na magaidi wa Daesh

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema serikali yake itatafanya kila liwezekanalo ili kukomesha kikamilifu mashambulizi na harakati za kundi la kigaidi na kitakfiri la Desh (ISIS) nchini humo.

Hollande ametoa kauli hiyo baada ya watu watatu kuuawa kanisani kaskazini mwa nchi hiyo ya Ulaya. Hollande amesema kuwa, "Kundi la kigaidi la ISIS limetangaza vita dhidi ya Ufaransa na kwamba Paris haina budi kutumia kila njia ili kuwaangamiza maadui hao kwa kuheshimu sheria zilizopo."

Maafisa wa polisi nje ya Kanisa la St-Etienne-du-Rouvray eneo la Normandy, Ufaransa baada ya magaidi wa Daesh kulivamia na kuwashikilia mateka wafuasi wa kanisa hilo.

Kasisi wa kanisa hilo la kikatoliki la St-Etienne-du-Rouvray lililoko kusini mwa mji wa Rouen eneo la Normandy, kaskazini mwa Ufaransa, aliuawa kwa kuchinjwa baada ya watu wawili waliokuwa na visu kuwashikilia mateka wafuasi wa kanisa hilo kwa masaa kadhaa. Hata hivyo baadaye maafisa usalama walifanikiwa kuwaua wavamizi hao kwa kuwafyatulia risasi. 

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki

Wakati huohuo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelaani mauaji hayo aliyoyataja kuwa ya kikatili na ya kutisha na kusema kuwa, lengo la hujuma hiyo dhidi ya eneo l ibada ni kuzusha woga na wasiwasi miongoni mwa binadamu.

Wahanga wa hujuma ya Nice, Ufaransa

Itakumbukwa kuwa, watu wasiopungua 84 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanyika Julai 14 katika mji wa pwani wa Nice nchini Ufaransa, baada ya mtu mmoja aliyekuwa ndani ya lori kugonga umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika maadhimisho ya Fataki ya Siku ya Kitaifa ya Bastille.

Aidha watu zaidi ya 130 waliuwa katika wimbi la mashambulizi ya kigaidi katika maeneo sita tofauti katika mji mkuu Paris Novemba mwaka jana.

Tags