Maandamano ya Kwanza Dhidi ya Sera za Trump huko Washington
Wakati ambapo Donald Trump, rais mteule wa Marekani, ameapishwa rasmi Jumatatu, tarehe 20 Januari, maandamano dhidi ya sera zake tayari yameanza. Katika muktadha huu, maelfu ya Wamarekani, wengi wao wakiwa wanawake, wamekusanyika katika mitaa ya Washington kuandamana dhidi ya sera za Trump.
Maandamano haya ya kwanza, yaliyofanyika Jumamosi yalihudhuriwa na wanaharakati wa haki za wanawake, watetezi wa haki za kijamii, na makundi mengine. Kwa mujibu wa waandaji, kulikuwa na waandamanaji wapatao 50,000, lakini polisi wa eneo hilo walitaka kuyadunisha na hivyo walidai kwamba yalihudhuriwa na watu takriban 25,000. Washiriki wa maandamano hayo walipinga sera mbalimbali za Trump ikiwa ni pamoja na sera zake dhidi ya wahamiaji, demokrasia, mabadiliko ya tabianchi, na pia msimamo wake kuhusu vita vya Gaza. Maandamano mengine kama hayo yamefanyika Jumatatu siku ambayo Trump.
Viongozi wa haki za kiraia wameahidi kuendelea kuhamasisha watu kupinga sera za Trump. Mtawala mpya wa Marekani ameahidi kufanya mabadiliko makubwa punde katika siku za awali za urais wake, ikiwa ni pamoja na sera za kuwatimua wahamiaji na kuvunja baadhi ya idara za serikali ya shirikisho. Kwa kuwa chama cha Republican, ambacho kinamuunga mkono Trump, kinaongoza Bunge la Marekani (Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti), na wahafidhina wana ushawishi mkubwa katika Mahakama Kuu ya Marekani, uwezo wa wanaharakati wa kisiasa na kijamii au wapinzani wa chama cha Democrat kupinga mipango ya Trump unatia shaka au utakuwa dhaifu.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Trump alisisitiza kuwa, akishinda na kufika Ikulu ya Marekani, atakuwa "dikteta," ingawa alisema hali hiyo ingetokea tu "siku ya kwanza." Sasa macho yote yameelekezwa kwake kuona jinsi atakavyotumia mamlaka yake akiwa Ikulu.

Inatarajiwa kwamba Trump atatoa idadi kubwa ya maagizo ya kiutendaji katika siku za awali za urais wake, jambo ambalo si geni kwa marais wapya. Hata hivyo, maagizo haya yanaweza kukabiliwa na changamoto za kisheria au za Bunge. Trump ametoa ahadi takriban 60 za kutekelezwa katika siku za awali za urais wake, na inakadiriwa kwamba atatoa maagizo ya kiutendaji karibu 100.
Miongoni mwa ahadi muhimu za Trump katika siku za awali za utawala wake ni kuwafukuza wahamiaji walioko Marekani kinyume cha sheria. Trump amesema atatangaza "hali ya dharura ya kitaifa" na kutumia jeshi kutekeleza mpango huo. Ahadi hii ya Trump imekosolewa vikali ndani na nje ya Marekani. Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, ameonya kwamba mpango huo wa kufukuza wahamiaji kwa wingi utakuwa "janga."
Trump pia ameahidi kuanza kutoa msamaha wa rais kwa wafuasi wake waliokamatwa kufuatia uvamizi wa jengo la Bunge la Marekani mnamo Januari 6, 2021, akiwaita "wafungwa wa kisiasa" na "mateka." Vurugu hizo zilitokea baada ya Trump kukata matokeo ya uchaguzi wakati huo.

Katika sera za kiuchumi, Trump amepanga kuongeza ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nchi washirika, zikiwemo bidhaa za China, ambapo ushuru unaweza kufikia asilimia 60. Pia, anapanga kuondoa kanuni kali katika sekta za viwanda, akisema kuwa kanuni hizo zinaongeza gharama kwa watumiaji wa Marekani.
Katika sera za kigeni, Trump amekuwa akikosoa vikali utawala wa Biden kuhusu namna Marekani ilivyoondoa askari wake Afghanistan. Ameahidi kuwawajibisha waliohusika katika mchakato huo. Pia, Trump amedai kuwa, endapo angekuwa rais, vita vya Ukraine na Gaza visingetokea.
Kwa kuzingatia hali hii, inatarajiwa kuwa siku 100 za kwanza za urais wa Trump katika awamu yake ya pili zitakuwa zenye dhoruba na changamoto nyingi, zikileta migogoro ya kisiasa na kijamii nchini Marekani na changamoto katika sera za kigeni za nchi hiyo.