Uroho wa Trump katika muhula wa pili wa urais wake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121950-uroho_wa_trump_katika_muhula_wa_pili_wa_urais_wake
Rais Donald Trump wa Marekani ameanza muhula wake wa pili wa uongozi huku akiweka hadharani uroho wake wa kupora ardhi, biashara na fedha za mataifa mengine ambapo ametangaza wazi azma yake ya kutaka kunyakua na kuunganisha ardhi za nchi huru na Marekani na pia kuhodhi kandarasi zenye faida kubwa kutoka kwa washirika wa Washington.
(last modified 2025-01-27T04:41:18+00:00 )
Jan 27, 2025 04:41 UTC
  • Uroho wa Trump katika muhula wa pili wa urais wake

Rais Donald Trump wa Marekani ameanza muhula wake wa pili wa uongozi huku akiweka hadharani uroho wake wa kupora ardhi, biashara na fedha za mataifa mengine ambapo ametangaza wazi azma yake ya kutaka kunyakua na kuunganisha ardhi za nchi huru na Marekani na pia kuhodhi kandarasi zenye faida kubwa kutoka kwa washirika wa Washington.

Kuhusiana na hilo, Trump kwa mara nyingine tena ameweka wazi uroho wake kuhusu Kanada ambapo ametaka kudhibitiwa kwa rasilimali za nchi hiyo na kuunganishwa ardhi yake na Marekani. Akizungumza katika safari yake ya karibuni huko North Carolina, alitoa wito kwa Kanada kujiunga na kuwa jimbo la 51 la Marekani na kudai kuwa iwapo itajiunga na Marekani, raia wake watafaidika na misamaha mikubwa ya kodi, forodha na kunufaika na huduma za hali ya juu za afya. Hata hivyo, Kanada imepinga msimamo huo wa Trump na kudai kuzingatia uhuru na utambulisho wake wa kitaifa.

Pia, Rais wa Marekani alikuwa na mvutano na Waziri Mkuu wa Denmark kuhusu Greenland na tamaa ya Marekani ya kutaka kulidhibiti eneo hilo. Simu ya dakika 45 kati ya Donald Trump na Matte Fredriksen mnamo Januari 15 iliibua mabishano makali ya maneno kati ya pande hizo. Trump, ambaye alikuwa rais mteule wa Marekani wakati huo, alichukua msimamo mkali na kutishia kumtoza ushuru mshirika huyo wa Marekani katika NATO. Wakati huo, Waziri Mkuu wa Denmark alirejelea kauli za Spika wa Bunge la Greenland kwamba kisiwa hicho hakiuzwi na kwamba ni Greenland ambayo inapaswa kuamua kuhusu mustakbali wake.

Wakati huo huo, Donald Trump ameongeza matakwa yake ya kifedha na kibiashara katika siku za kwanza kabisa za kuingia kwake Ikulu ya White House. Takwa lake la kwanza katika uwanja huo lilielekezwa moja kwa moja kwa mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta duniani, Saudi Arabia. Trump alisema kuwa ataiomba Riyadh kuwekeza kati ya dola milioni 600 na trilioni 1 nchini Marekani, ili kupunguza bei ya mafuta na wakati huo huo kutoa mashinikizo dhidi ya Russia. Alidai kuwa kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya OPEC kunaweza kuathiri moja kwa moja na hatimaye kumaliza vita vya Ukraine. Baada ya mazungumzo ya simu na Trump, Mohammed bin Salman Mwanamfalme wa Saudia alisisitiza kuwa Riyadh inapanga kuongeza uwekezaji wake na uhusiano wa kibiashara na Marekani hadi kufikia dola bilioni 600 katika miaka minne ijayo, na kwamba ikiwa fursa zaidi zitatolewa, idadi hii inaweza kuongezeka.

Trump na Netanyahu wanahatarisha amani na usalama wa dunia

Wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Trump, Saudi Arabia ilitia saini mikataba ya kiuchumi, kibiashara na kijeshi ya  jumla ya karibu dola bilioni 500 na Marekani, ambapo Trump alisema wakati wa kampeni zake za uchaguzi kwamba Saudi Arabia ni kama ng'ombe wa kukamwa. Alikwenda Riyadh katika safari yake ya kwanza ya nje ya nchi na kuanzisha mgogro wa Qatar. Sasa, Trump amesema kuwa yuko tayari kwenda tena Saudi Arabia katika safari yake ya kwanza ya nje katika muhula wa pili wa urais wake iwapo kandarasi zenye thamani ya dola bilioni 600 na nchi hiyo ya Kiarabu zitatiwa saini.

Misimamo na kauli za Trump zinaonyesha nia yake ya kuzitwisha nchi nyingine matakwa ya Marekani. Katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 2020, Trump alitangaza kwamba Merika "itatumikia hatima yake kama mpenda amani, lakini amani hupatikana kwa nguvu." Hii ina maana ya kuvuruga utaratibu wa kimataifa wa kisiasa, kijiografia, kiuchumi na kibiashara na kuhatarisha amani ya kieneo na kimataifa. Katika uwanja huo wakosoaji wa Donald Trump wanamtuhumu kuwa anawadhalilisha washirika wa Marekani na kudhoofisha miungano na Washington. Wanatabiri kuwa chini ya utawala wa pili wa Trump, Marekani itaendelea kutengwa kimataifa na hivyo kudhuru maslahi ya Marekani na kuhatarisha amani duniani.

Rais Trump, katika muhula wake wa kwanza wa uongozi kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2021, sambamba na kauli mbiu yake ya uchaguzi ya, "Marekani Kwanza" na kwa kisingizio cha kurejesha mamlaka ya nchi, katika nyanja za kisiasa, kijeshi na kiusalama, aliwashinikiza washirika wa NATO Ili kuongeza sehemu ya gharama za kijeshi hadi asilimia mbili ya pato la ndani la nchi wanachama. Sasa anataka kuongeza matumizi ya kijeshi ya wanachama wa NATO hadi asilimia 5 ya pato lao la Taifa. Katika uwanja wa biashara, Trump pia alitekeleza hatua zenye utata za kuegemea upande mmoja na, huku akikataa makubaliano ya biashara ya kimataifa, aliweka ushuru mkubwa wa forodha kwa uingizaji wa bidhaa nchini Marekani ili kufidia nakisi ya kibiashara ya Marekani, ambayo kwa mtazamo wake ni ishara ya udhaifu wa Marekani katika uwanja huo. Matamshi na vitisho vya Trump mwanzoni mwa muhula wa pili wa urais wake vinaashiria kutekelezwa tena kwa sera hizo hizo. Hata hivyo, mtazamo wake katika masuala hayo umeongeza mivutano ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi kati yake na jamii ya kimataifa. Kuendelea kwa siasa zake hizo bila shaka kutaongeza tofauti za Marekani na nchi nyingine na kuibua mivutano mfululizo kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa.