Waziri Mkuu wa Italia achunguzwa kwa kumuachia huru mshukiwa wa ICC
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni amewekwa chini ya uchunguzi wa mahakama kufuatia uamuzi wa serikali yake wa kumwachilia huru afisa wa polisi wa Libya anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Osama Elmasry Njeem aliachiliwa huru wiki iliyopita na kurudishwa nyumbani kwa ndege ya serikali ya Italia, siku chache baada ya kuzuiliwa katika mji wa kaskazini wa Turin chini ya waranti wa kukamatwa wa ICC, akikabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso na ubakaji.
Mahakama ya ICC imesema inataka maelezo kutoka kwa serikali ya Italia, ikisisitiza kuwa haikushauriwa kuhusu uamuzi wa kumwachilia huru afisa huyo wa Libya.
Meloni alisema katika ujumbe aliotuma kwenye mitandao ya kijamii jana Jumanne kwamba, aliwekwa chini ya uchunguzi na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Roma, Francesco Le Voi, kwa madai ya kusaidia uhalifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kisheria, Meloni hana wajibu wa kujiuzulu. Kuwekwa chini ya uchunguzi nchini Italia haimaanishi ana hatia, wala haimaanishi kwamba lazima atafungulia mashtaka rasmi.
Waziri wa Sheria, Carlo Nordio, Waziri wa Mambo ya Ndani, Matteo Piantedosi na waziri msaidizi katika maswala ya kijasusi, Alfredo Mantovano pia wamewekwa chini ya uchunguzi, Meloni ameongeza.