Maelfu waandamana Washington kupinga sera za uhamiaji za Trump
Maelfu ya watu huko Marekani wamefanya maandamano nje ya Ikulu ya White House mjini Washington DC, kupinga mpango wa Rais wa nchi hiyo, Donald Trump wa kusimamisha ufadhili wa serikali, pamoja na sera zake tata za uhamiaji.
Waandamanaji hao wamepaza sauti na kutoa nara kama vile "Hivi ndivyo demokrasia inavyoonekana" na kushikilia mabango yaliyosomeka "Achia Fedha" walipokuwa wakiandamana nje ya Ikulu ya White House Jumanne, kufuatia uamuzi wa Trump wa kusitisha matrilioni ya dola za ufadhili wa serikali ya nchi hiyo.
Uamuzi huo tata Trump umezusha malalamiko na upinzani mkubwa kote nchini Marekani, huku Democrats wakiapa kupinga hatua hiyo kupitia njia za kisheria.
Utawala wa Trump ulitangaza kusitisha ruzuku na mikopo ya serikali ya shirikisho, na hivyo kusababisha mkanganyiko mkubwa katika serikali, Congress, mipango ya serikali na mashirika yasiyo ya serikali ambayo yanategemea ufadhili huo.
Wakosoaji wanaonya kuwa, agizo hilo tatanishi la serikali mpya yaTrump linaweza kuvuruga shughuli za elimu, huduma za afya, mipango ya kupunguza umaskini na kukabiliana na majanga.
Maafisa katika utawala wa Trump wanadai kuwa, kusitishwa kwa ufadhili ni muhimu ili kuhakikisha kuwa ufadhili wote unaendana na vipaumbele vya kiongozi huyo aliyeapishwa kuhudumu kwa muhula wa pili mnamo Januari 20.