Ufaransa: Kesi ya Sarkozy na "dili" la nyuma ya pazia na Gaddafi yaendelea
Kesi inayoendelea kwa miezi kadhaa ya rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy kuhusu madai ya kufadhili kampeni yake ya urais mwaka 2007 kinyume cha sheria, sasa imeangazia mazungumzo ya siri ya Ufaransa na serikali ya kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi.
Wanafamilia wa wahanga wa mashambulizi yanayodaiwa kufanyika kwa amri ya utawala wa Gaddafi, wameiambia mahakama kuwa wanamshuku Bw. Sarkozy kuwa alikuwa tayari kutoa mhanga kumbukumbu za wapendwa wao ili kurejesha uhusiano na Libya, karibu miaka 20 iliyopita.
Waendesha mashtaka wa Ufaransa Alhamisi iliyopita waliomba kifungo cha miaka saba jela kwa kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 70. Bwana Sarkozy, ambaye alikuwa rais wa Ufaransa kuanzia 2007 hadi 2012, amekanusha makosa yote yanayomkabili.
Kesi hiyo iliyoanza Januari, imepangwa kuendelea hadi Aprili 8, huku mawakili wa Sarkozy wakitarajiwa kuwasilisha hoja zao siku ya mwisho. Uamuzi wa kesi hiyo unatarajiwa baadaye.
Baadhi ya nyakati muhimu katika kesi hiyo zinamulika mazungumzo kati ya Ufaransa na Libya katika miaka ya 2000, wakati Gaddafi alipotaka kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na nchi za Magharibi. Kabla ya hapo, Libya ilitambuliwa kuwa nchi iliyotengwa na nchi za Magharibi kwa madai kufadhili mashambulizi ya kigaidi.
Familia za Wfaransa wahanga wa shambulio la bomu mwaka 1989 zimeieleza mahakama mshtuko wao na hisia za kusalitiwa wakati kesi hiyo ikijadili kama ahadi zilizotolewa kwa serikali ya Gaddafi zilikuwa sehemu ya madai ya mpango wa rushwa.
Mnamo 1988, bomu lililolipuka katika ndege ya Pam Am katika anga ya mji wa Lockerbie huko Scotland, liliua watu 270 na wengine 21 waliokuwa chini ardhini, wakiwemo Wamarekani 190.
Uchunguzi wa Ufaransa na Marekani ulihusisha mashambulizi hayo na Libya, ambayo wakati huo serikali yake ilikuwa katika uhasama wa muda mrefu na Marekani na nchi nyingine za Magharibi.
Sasa, familia za wahasiriwa zinashangaa kama maafisa wa serikali ya Ufaransa walio karibu na Sarkozy wameahidi kusahau mashambulizi hayo ili kupata fursa za kibiashara na nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta na pengine, kesi inayodaiwa kuwa ya ufisadi.