Mtaalamu: Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kudhoofisha uchumi wa dunia katika siku zijazo
Erhan Aslanoglu, Profesa katika Chuo Kikuu cha Bilgi mjini Istanbul, Uturuki ameeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yatababisha kuzorota kwa uchumi wa dunia katika siku zijazo, kuathiri uzalishaji n.k.
Profesa Aslanoglu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi amesema, athari za mabadiliko ya hali ya hewa au tabianchi kwa viwanda, utalii, na kilimo si tu kwamba huathiri mazingira bali pia viashiria vya kiuchumi.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha New South Wales nchini Australia kuhusu mfungamano wa uchumi wa dunia na tatahira za mabadiliko ya tabia nchi kutoka nchi moja hadi nyingine umeonyesha kuwa makadirio ya hasara ya uchumi mkuu yalikuwa mabaya zaidi kulingana na mazingira ya utoaji wa gesi chafuzi.
Profesa Erhan Aslanoglu ameongeza kuwa: Mabadiliko ya hali ya tabianchi huathiri moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja shughuli za kiuchumi lakini watu kupoteza maisha ndio kipengele muhimu zaidi, kwani kupanda kwa joto kunaweza kusababisha matatizo ya kiafya, kama vile mshtuko wa moyo na shinikizo la damu.
"Licha ya kuwa ni vigumu sana kupima, matatizo haya ya kiafya yanaweza kutokana na hali ya hewa, ndiyo maana tunapaswa kuainisha (athari za mabadiliko ya hali ya hewa) kama hasara ‘zinazoweza kupimika’ na ‘zisizoweza kupimika; joto la juu, majanga ya asili, na hali ya hewa ya baridi, yote haya husababisha hasara ya uzalishaji, ambayo ina gharama,” amesema Profesa Aslanoglu.
Amesisitiza kuwa uharibifu mkubwa unaosababishwa na dhoruba, mafuriko na ukame pia una gharama kubwa na kwamba nchi nyingi zinagharamika pakubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na wakati huo huo ni gharama na ni mzigo kwa sekta binafsi na sekta za umma.