China: Kusalimu amri kutachochea zaidi uchu wa Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amesema kusalimu amri na kufikia makubaliano na Marekani katika vita vya kibiashara vya Washington hakutakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuchochea zaidi uchu na uroho wa Marekani.
Wang Yi alisema hayo wakati wa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la BRICS mjini Rio de Janeiro, nchini Brazil, kwa mujibu wa shirika la habari la TASS la Russia.
Yi ameeleza kuwa, "Marekani kwa muda mrefu imenufaika sana kutokana na biashara huria, lakini sasa inatumia ushuru wa forodha kama njia ya kuzipandishia bei nchi nyingine."
Ameeleza bayana kuwa: Ikiwa tutasalimu amri na kufikia makubaliano kimya kimya, mnyanyasaji (Marekani), baada ya kupata inchi (moja), atataka sasa kuchukua maili tatu," Waziri Yang amesema, akinukuliwa na tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China.
Haya yanajiri huku Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ukitahadharisha kuwa, mfumo wa fedha wa kimataifa umelemewa na mashinikizo makubwa, kwa sababu vita vya kibiashara vya Rais Donald Trump wa Marekani vinavyoyumbisha masoko ya fedha.

Kadhalika Shirika la Biashara Duniani (WTO) lilitahadharisha hivi karibuni kuwa, ushuru uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump utarudisha nyuma biashara ya kimataifa mwaka huu na kupelekea kushuka kwa kasi ukuaji wa uchumi wa dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesisitiza kuwa, kudumisha na kuheshimu sheria za biashara ya kimataifa ndicho kipaumbele na suala muhimu zaidi kwa Beijing hivi sasa.