Mauaji Gaza; Majaji, mawakili 800 wa UK wataka Israel ifukuzwe UN
Kundi la mawakili waandamizi, majaji wa zamani na wasomi wengine zaidi ya 800 wa Uingereza wameitaka serikali ya London kuuwekea vikwazo utawala wa Israel, na kushinikiza kusimamishwa uanachama wa Tel Aviv katika Umoja wa Mataifa.
Mwito huo upo katika barua aliyoandikiwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer jana Jumanne na mamia ya mawakili waandamizi, majaji wa zamani na wasomi wa nchi hiyo.
"Mawaziri wa Israel na maafisa wakuu wa kijeshi lazima wawekewe vikwazo mara moja," waraka huo umesema ukiwashutumu maafisa hao kwa kuchochea mauaji ya halaiki na kufadhili ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni.
Wasomi hao wa Uingereza wameishutumu Israel kwa kutekeleza uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu dhidi ya Wapalestina.
Barua hiyo imeonya kwamba, kuna ushahidi mkubwa wa mauaji ya kimbari huko Gaza. Imenukuu matamshi ya hivi karibuni ya Bezalel Smotrich, waziri wa mrengo wa kulia wa Israel, ambaye alisema jeshi la utawala huo "litafuta" uwepo wa Wapalestina huko Gaza.
Wamesema Starmer lazima achukue "hatua za haraka na madhubuti bila kuchelewa, ili kuepusha maangamivu ya watu wa Palestina wa Gaza."
"Mataifa yote, ikiwa ni pamoja na Uingereza, yanalazimika kisheria kuchukua hatua zinazofaa ndani ya uwezo wao kuzuia na kuadhibu wahusika wa mauaji ya halaiki; kuhakikisha sheria za kimataifa za kibinadamu ziheshimiwa; na kukomesha ukiukaji wa (haki ya kujitawala)," barua hiyo imesema.