Balozi wa Colombia: Dunia isifumbie macho mateso ya watu wa Gaza
Jorge Ivan Ospina, balozi mpya wa Colombia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amesema "ulimwengu haupaswi kuwafumbia macho" raia wa Palestina wanaoteseka huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.
Ospina alisema hayo jana Jumatatu na kuongeza kwamba, Colombia iko tayari kutoa matibabu kwa maelfu ya Wapalestina waliojeruhiwa katika vita vya Israel dhidi ya Gaza. "Watu hawawezi kufa kwa njaa. Ni lazima wapate matibabu ya haraka na lazima washughulikwe," ameongeza Ospina.
Katika ujumbe wake huo, Ospina alitangaza hadharani kuteuliwa kwake na kumshukuru Rais Gustavo Petro wa Colombia na Waziri wa Mambo ya Nje, Laura Sarabia kwa uteuzi huo. Ameshutumu vikali "mauaji ya halaiki ambayo Wapalestina wanakumbana nayo leo hii" akisisitiza kuwa atafanya juhudi kuelekea "uhuru wa watu wanaoishi huko (Palestina)."
Uteuzi huo unaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uamuzi wa Colombia wa kulitambua rasmi taifa la Palestina mnamo mwaka 2018. Colombia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka jana kutokana na vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza.

Mwezi uliopita, Rais wa Colombia, Gustavo Petro alikashifu "mauaji ya umwagaji damu" ya utawala wa Israel huko Gaza, akishabihisha masaibu ya Wapalestina na mateso ya Nabi Isa Masih (Yesu).
Kiongozi huyo wa Colombia amekuwa mkosoaji mkubwa wa kampeni ya mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza, na mara kwa mara amekuwa akiukosoa utawala wa Kizayuni kwa jinai zake za kivita huko Gaza, ambapo Wapalestina wapatao 54,000 wameuawa.