Washington yakasirishwa na kufichuliwa ripoti ya siri ya uongo wa Trump kuhusu Iran
(last modified Thu, 26 Jun 2025 15:58:01 GMT )
Jun 26, 2025 15:58 UTC
  • Washington yakasirishwa na kufichuliwa ripoti ya siri ya uongo wa Trump kuhusu Iran

Kufichuliwa ripoti ya siri kuhusu kufeli mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kumewakasirisha maafisa wa serikali ya Washington.

Gazeti la Wall Street Journal limeripoti likimnukuu Waziri wa Ulinzi wa Marekani kwamba, Ofisi ya Polisi ya Upelelezi ya Marekani, FBI imeanza uchunguzi kuhusu jinsi ripoti za kijasusi za matokeo ya mashambulizi ya nchi hiyo dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, zilivyovujishwa.

Televisheni ya CNN imeripoti kuwa, vyanzo vitatu vyenye taarifa ya tathmini ya awali ya ujasusi ya Marekani vimeripoti kuwa mashambulizi ya kijeshi ya nchi hiyo kwenye vituo vitatu vya nyuklia vya Iran wiki iliyopita hayakuharibu sehemu muhimu za mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, na kwamba kuna uwezekano wa kuchelewesha mpango huo kwa miezi michache tu.

Tathmini hiyo ambayo haikuripotiwa hapo awali imetayarishwa na Shirika la Ujasusi la Ulinzi (DIA), ambalo ni kitengo cha ujasusi cha Pentagon. Chanzo kimoja kinasema, uchambuzi huo ulitokana na tathmini ya uharibifu iliyofanywa na Kamandi Kuu ya Marekani katika Mashariki ya Kati (CENTCOM) baada ya mashambulizi hayo.

Uchambuzi wa uharibifu wa maeneo hayo na athari za mashambulizi dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran unaendelea na huenda ukabadilika kadiri taarifa zaidi zinavyopatikana, lakini matokeo ya awali yanakinzana na madai ya mara kwa mara ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba mashambulizi hayo yaliharibu kabisa nyenzo za kurutubisha madini ya urani nchini Iran.

Vyanzo viwili vilivyosoma tathmini hiyo vimesema kwamba hifadhi ya Iran ya madini ya uranium iliyorutubishwa haijaharibiwa, na kwamba mashinepewa (centrifuges) zimebakia kwa kiasi kikubwa. Kwa msingi huo, tathmini inaonyesha kuwa, zaidi ni kwamba Marekani imerudisha nyuma mpango wa Iran kwa miezi michache tu.