Waliofariki kwa mafuriko katika jimbo la Texas nchini Marekani yafikia 104
Duru kadhaa za habari zimeripoti kuwa idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko yaliyotokea katika jimbo la Texas nchini Marekani imeongezeka na kufikia 104.
Kwa mujibu wa chaneli ya NBC, Kaunti ya Kerr imeshuhudia vifo 84 kutokana na mafuriko hayo, wakiwemo watu wazima 56 na watoto 28, wakati 15 kati ya watu wazima na tisa kati ya watoto waliofariki wakiwa bado hawajatambuliwa.
Chaneli ya CBS imeripoti kuwa, mbali na vifo vilivyothibitishwa, watoto 10 na mshauri mmoja kutoka Camp Mystic, ambayo ni kambi ya kidini ya wasichana wa Kikristo iliyoko karibu na Hunt magharibi mwa Kaunti ya Kerr.
Siku ya Jumatatu, kambi hiyo ya kidini ya majira ya joto ilitangaza kuwa wapiga kambi na washauri 27 wamefariki dunia katika mafuriko.
CNN imetangaza kuwa, vifo zaidi vimeripotiwa katika kaunti nyingine kadhaa, saba kati yao katika Kaunti ya Travis, vinne katika Kaunti ya Burnet, sita katika Kaunti ya Kendall, mbili katika Kaunti ya Williamson, na moja katika Kaunti ya Tom Green.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amekanusha madai kwamba taasisi ya Huduma ya Taifa ya Hali ya Hewa ilishindwa kutoa indhari za kutosha na kwa wakati kuhusu mafuriko.
Gazeti la New York Times hapo awali liliripoti kuwa, nyadhifa kadhaa muhimu katika taasisi ya Huduma ya Taifa ya Hali ya Hewa zilikuwa tupu kutokana na kupunguzwa bajeti yake na Trump baada ya kuingia madarakani, na kueleza kwamba ombwe hilo huenda ndilo lililokwamisha kuchukuliwa hatua za dharura.
Mafuriko hayo yalianza mwishoni mwa Alkhamisi iliyopita na kuendelea hadi saa za alfajiri ya Ijumaa, huku mvua kubwa ikinyesha kwenye Mto Guadalupe, na kuusukuma hadi kwenye kingo kwa kina cha zaidi ya mita 11.8.../