CNN: Vita vya Ukraine sasa ni vita vya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129170-cnn_vita_vya_ukraine_sasa_ni_vita_vya_trump
Rais Donald Trump wa Marekani ameingia kikamilifu katika vita vya Ukraine na kushika usukani wa mgogoro huo kisiasa na kijeshi; vita ambavyo, katokana na maamuzi yake ya karibuni sio tena mzozo wa kikanda, bali ni mtihani kuhusu nafasi ya Marekani duniani.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Aug 05, 2025 14:12 UTC
  • CNN: Vita vya Ukraine sasa ni vita vya Trump

Rais Donald Trump wa Marekani ameingia kikamilifu katika vita vya Ukraine na kushika usukani wa mgogoro huo kisiasa na kijeshi; vita ambavyo, katokana na maamuzi yake ya karibuni sio tena mzozo wa kikanda, bali ni mtihani kuhusu nafasi ya Marekani duniani.

Wakati Donald Trump anakaribia makataa yake ya siku 100 kufikiwa amani nchini Ukraine, mashinikizo yake kwa Russia, kwa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) na hata kwa wateja wa nishati ya Moscow kama India na China yamefikia katika kipindi nyeti.  

Hivi sasa Rais wa Marekani si tu anawajibika kwa ahadi ya amani aliyoitoa, lakini pia kwa matokeo yote ya vita.

CNN imeandika kuwa: Trump amepewa jukumu la kusimamia mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia, kwa sababu Marekani ilihusika katika vita hivyo kama mshirika mkuu na muungaji mkono wa Ukraine chini ya Rais aliyetangulia. 

CNN imeongeza kuwa: Trump angeweza kujiondoa kikamilifu katika vita vya Ukraine, lakini badala yake amechagua kushika usukani wake kwa kulazimisha matakwa na ushawishi wake binafsi. Awali alidhani kuwa angeweza kuvimaliza ndani ya "saa 24" au katika kipindi cha siku 100.

Hata hivyo, maamuzi aliyochukua Rais wa Marekani katika kipindi cha wiki mbili za karibuni yamefanya suala hili kuwa tatizo ambalo sasa ni lake binafsi.