Orban: Hungary haitaruhusu Ukraine kujiunga na EU miaka 100 ijayo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135822-orban_hungary_haitaruhusu_ukraine_kujiunga_na_eu_miaka_100_ijayo
Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban amesema kwamba Ukraine inajaribu kushawishi na kuathiri matokeo ya uchaguzi ujao wa bunge nchini Hungary, akisitiza kuwa nchi yake haitaruhusu Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya katika miaka 100 ijayo.
(last modified 2026-01-23T23:17:54+00:00 )
Jan 23, 2026 23:17 UTC
  • Orban: Hungary haitaruhusu Ukraine kujiunga na EU miaka 100 ijayo

Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban amesema kwamba Ukraine inajaribu kushawishi na kuathiri matokeo ya uchaguzi ujao wa bunge nchini Hungary, akisitiza kuwa nchi yake haitaruhusu Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya katika miaka 100 ijayo.

Viktor Orban amesema hayo katika mkutano wa waandishi wa habari, akitoa maoni yake kuhusu matokeo ya mkutano wa kilele wa EU huko Brussels na kueleza kuwa, Ukraine inajaribu kushawishi matokeo ya uchaguzi ujao wa bunge nchini Hungary kwa sababu inajua serikali ya sasa haitairuhusu ijiunge na EU.

Katika mkutano huu mjini Brussels, Kamisheni ya Ulaya ilisambaza ramani ya njia ya kujiunga Ukraine na umoja huo ifikapo mwaka wa 2027.

Orban akizungumzia mpango huo, amesema, "Nadhani kwamba katika miaka mia moja ijayo, hatutakuwa na bunge nchini Hungary ambalo litapigia kura kuidhinisha kujiunga Ukraine na EU."

"Hatutaki wajiunge na EU," Waziri Mkuu wa Hungary amesema na kuongeza kuwa, hii ndiyo sababu Kiev inavutiwa na ushindi wa upinzani na inajaribu kuingilia mambo ya ndani ya Budapest.

Ameongeza kuwa, "Lazima tukubali kwamba, Waukraine watakuwa washiriki hai katika kampeni ya [uchaguzi] ya Hungary kwa sababu ni kwa maslahi yao ya msingi kubadilisha serikali nchini Hungary. Sifurahii jambo hili, na tutapambana nalo." 

Kwa mujibu wa maafisa wa Hungary, "Waliberali wa Ulaya wanaounga mkono vita" wanakwamisha kufanyika mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Russia ili kuhitimisha vita huko Ukraine.