Putin: Wanajeshi wa NATO nchini Ukraine watakuwa 'shabaha halali' ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130444-putin_wanajeshi_wa_nato_nchini_ukraine_watakuwa_'shabaha_halali'_ya_russia
Rais Vladimir Putin wa Russia amepinga mapendekezo ya 'dhamana ya usalama ya nchi za Magharibi kwa Ukraine' akionya kwamba, wanajeshi wowote wa kigeni watakaotumwa katika nchi hiyo jirani watakuwa "shabaha halali" ya jeshi la Russia.
(last modified 2025-09-05T11:03:21+00:00 )
Sep 05, 2025 11:03 UTC
  • Putin: Wanajeshi wa NATO nchini Ukraine watakuwa 'shabaha halali' ya Russia

Rais Vladimir Putin wa Russia amepinga mapendekezo ya 'dhamana ya usalama ya nchi za Magharibi kwa Ukraine' akionya kwamba, wanajeshi wowote wa kigeni watakaotumwa katika nchi hiyo jirani watakuwa "shabaha halali" ya jeshi la Russia.

Akizungumza katika Jukwaa la Kiuchumi la Mashariki huko Vladivostok, Putin ametoa indhari hiyo,  akijibu mapendekezo ya mkutano wa waungaji mkono wa Ulaya wa Ukraine - uliopewa jina la "muungano wa wenye irada" huko Paris. Amesisitiza upinzani wa Moscow kwa mapendekezo ya kundi hilo la kutumwa wanajeshi wa NATO nchini Ukraine.

"Nchi za Magharibi kuiburuza Ukraine katika NATO ilikuwa moja ya sababu za kuibuka mzozo uliopo. Ikiwa wanajeshi wowote watajitokeza sasa (Ukraine), wakati mzozo huu unapoendelea, tutawatambua kuwa shabaha halali ya kijeshi," Putin ameonya.

Onyo la Putin limekuja siku moja baada ya mataifa kadhaa kuahidi kutuma wanajeshi katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita, eti kama dhamana ya usalama kwa makubaliano ya amani yanayotarajiwa kusainiwa kati ya Moscow na Kyiv.

Rais wa Russia amesisitiza kuwa: Wanajeshi wowote wa Magharibi watakaotumwa Ukraine wanaweza kuwa walengwa halali wa vikosi vya Russia au kutokuwa na umuhimu katika suala la makubaliano ya amani.

Wakati huo huo, Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin), Dmitry Peskov amesema kuwa pendekezo lililokubaliwa katika mkutano wa kilele wa Paris "halikubaliki" kabisa. "Tunautazama kama tishio kwetu - uwepo wa vikosi vya kimataifa, au vikosi vyovyote vya kigeni, au vikosi vya NATO kwenye ardhi ya Ukraine, karibu na mpaka wetu," amewaambia waandishi wa habari.