Rais wa zamani wa Brazil ahukumiwa kifungo cha miaka 27 jela kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130708-rais_wa_zamani_wa_brazil_ahukumiwa_kifungo_cha_miaka_27_jela_kwa_kuhusika_na_jaribio_la_mapinduzi
Rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro amehukumiwa kifungo cha miaka 27 na miezi mitatu jela baada ya jopo la Mahakama Kuu kumpata na hatia ya kufanya jaribio la kuipindua serikali.
(last modified 2025-09-12T06:57:00+00:00 )
Sep 12, 2025 06:57 UTC
  • Rais wa zamani wa Brazil ahukumiwa kifungo cha miaka 27 jela kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi

Rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro amehukumiwa kifungo cha miaka 27 na miezi mitatu jela baada ya jopo la Mahakama Kuu kumpata na hatia ya kufanya jaribio la kuipindua serikali.

Majaji wanne kati ya watano wa jopo la mahakama hiyo jana Alkhamisi walipiga kura ya kumtia hatiani Bolsonaro kwa mashtaka yote matano yaliyokuwa yakimkabili katika kesi hiyo ya kihistoria.

Hukumu imetolewa wakati Majaji Carmen Lucia na Cristiano Zanin walipopiga kura kumpata Bolsonaro na hatia ya kupanga mapinduzi ili kusalia madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2022. Kura zao ziliunda wingi wa 4-1, wakiungana na wenzao Alexandre de Moraes na Flavio Dino, ambao walikuwa wamepiga kura ya utoaji hukumu mapema wiki hii. Kura moja ya upinzani ilitoka kwa Jaji Luiz Fux siku ya Jumatano, ambaye alipiga kura ya kumfutia Bolsonaro mashtaka yote.

Bolsonaro amepatikana na hatia ya kupanga njama ya mapinduzi, kushiriki katika shirika la uhalifu lililojizatiti kwa silaha, kujaribu kufuta utaratibu wa kidemokrasia wa Brazil kwa kutumia nguvu, kufanya vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya taasisi za serikali, na kuharibiwa na wafuasi wake mali ya umma iliyowekewa ulinzi katika hujuma waliyofanya dhidi ya majengo ya serikali mnamo Januari 8, 2023.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, njama hizo za mapinduzi zilijumuisha mpango wa kuwaua Rais Luiz Inacio Lula da Silva, Makamu wake Geraldo Alckmin na Jaji wa Mahakama ya Juu Alexandre de Moraes kwa kutumia viripuzi, silaha au sumu.

Jaji Carmen Lucia alisema, upande wa mashtaka ulitoa "ushahidi kamili" kwamba kikundi hicho, kinachoongozwa na Bolsonaro, kilitekeleza "mpango wa kisasa na wa kimfumo wa kushambulia taasisi za kidemokrasia."

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 70, ambaye kwa sasa yuko chini ya kizuizi cha nyumbani, amekana kufanya makosa yoyote. Mawakili wake wametangaza kwamba watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama Kuu yenye majaji wote 11.../