Waziri Mkuu wa Uhispania: Nasikitika hatuna bomu la nyuklia tukaizuia Israel isishambulie Ghaza!
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130714-waziri_mkuu_wa_uhispania_nasikitika_hatuna_bomu_la_nyuklia_tukaizuia_israel_isishambulie_ghaza!
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameendelea kukosoa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina huku akieleza kwa masikitiko kwamba Uhispania haina bomu la nyuklia, manowari ya kubebea ndege za kivita, wala utajiri mkubwa wa mafuta, vitu vitakavyoiwezesha kusimamisha peke yake mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Ghaza; lakini hiyo haimaanishi kwamba Madrid itasitisha juhudi zake.
(last modified 2025-09-12T06:58:12+00:00 )
Sep 12, 2025 06:58 UTC
  • Waziri Mkuu wa Uhispania: Nasikitika hatuna bomu la nyuklia tukaizuia Israel isishambulie Ghaza!

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameendelea kukosoa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina huku akieleza kwa masikitiko kwamba Uhispania haina bomu la nyuklia, manowari ya kubebea ndege za kivita, wala utajiri mkubwa wa mafuta, vitu vitakavyoiwezesha kusimamisha peke yake mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Ghaza; lakini hiyo haimaanishi kwamba Madrid itasitisha juhudi zake.

Sanchez, ameeleza hayo katika hotuba aliyotoa wakati akitangaza mipango yake ya baadaye kwa Uhispania na kusisitiza kwamba nchi hiyo inalaani jinai za Israel na kumshinikiza Netanyahu akomeshe jinai hizo dhidi ya binadamu.

Waziri Mkuu wa Uhispania amesema: "wanachofanya Wazayuni si kujilinda wala si kushambulia. Haya ni mauaji ya kimbari na kuwaangamiza watu kwa namna ya kishenzi zaidi. Huu ni ukiukaji wa sheria zote za kimataifa, hili ni janga."

Sanchez ameongezea kwa kusema: "mbali na sheria ya vikwazo vya uuzaji silaha kwa Israel ambayo serikali ya Uhispania imeitekeleza tangu Oktoba 2023, imepiga marufuku pia kupita kwenye bandari zake meli zinazoipelekea mafuta Israel. Hatua zingine za Uhispania ni pamoja na kususia bidhaa zinazozalishwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, na tumetangaza kwamba ni marufuku kuingia Uhispania mtu yeyote ambaye amehudumu au kuhusika moja kwa moja na mauaji ya kimbari huko Ghaza".

Matamshi ya Waziri Mkuu wa Uhispania ya kukosoa vitendo vya utawala ghasibu wa Israel, yametolewa baada ya watetezi na waungaji mkono wa Palestina kufunga barabara siku ya Jumatano wakati wa awamu ya 16 ya mashindano ya baiskeli ya Uhispania na kupelekea kusitishwa mashindano hayo. Watetezi hao wa Palestina walichukua hatua hiyo kupinga uwepo wa waendesha baiskeli wa utawala wa Kizayuni katika mashindano hayo; na kwa hatua yao ya kufunga njia, wakawazuia wasishiriki mashindano hayo.

Wakati huohuo, Waziri wa Utamaduni wa Uhispania Ernesto Ortason, ameonya kwamba ikiwa Israel itashiriki kwenye mashindano ya Tamasha la Nyimbo la Eurovision 2026, nchi yake itajiondoa kwenye mashindano hayo.

"Hatuwezi kuhalalisha kwa namna yoyote uwepo wa Israel katika matukio kama hayo, na kuonyesha kama kwamba hakuna chochote kinachojiri wakati huu," ameeleza Ortason katika mahojiano ya televisheni.../