Sarkozy ahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa uhalifu
Mahakama ya Paris jana Alhamisi ilimhukumu rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kifungo cha miaka mitano jela baada ya kumpata na hatia ya njama ya uhalifu katika kesi aliyotuhumiwa kwamba kiongozi zamani wa Libya mwendazake Muammar Gaddafi alisaidia kufadhili kampeni za Sarkozy katika uchaguzi wa rais mwaka 2007.
Mahakama hiyo ya Paris imeagiza Sarkozy kusalia rumande huku waendesha mashtaka wakipewa mwezi mmoja kumjulisha mkuu huyo wa zamani wa nchi lini anapasa kwenda jela. Uamuzi wa mahakama ya Paris unasalia mahala pake hata kama rais huyo wa zamani wa Ufaransa atakata rufaa kupinga hukumu dhidi yake.
Sarkozy, ambaye mara zote amekuwa akikana mashtaka hayo, alituhumiwa kufikia makubaliano na Gaddafi ili kupata kufadhiliwa kampeni zake za uchaguzi mkabala wa yeye kuiunga mkono serikali ya Libya ambayo wakati huo ilikuwa imetangwa kimataifa.
Jaji wa mahakama ya Paris ambaye alimfutia Nicolas Sarkozy baadhi ya mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ikiwemo ufisadi ameeleza kuwa hakuna uthibitibisho kwamba Sarkozy alifikia makubaliano hayo na Muammar Gaddafi wala pesa zilizokuwa zimetumwa kutoka Libya zilifika katika hazina za kampeni ya Sarkozy.
Jaji Nathalie Gavarino aidha amemuamuru Sarkozy kulipa fidia ya yuro laki moja.