China haina wasiwasi, bali inashangaa; mbona Marekani inang'ang'ania kurejea Afghanistan?
China imetangaza kwamba, njama za madola yaliyosababisha mgogoro wa Afghanistan za kujaribu kurejea nchini humo na kuweka kambi zao za kijeshi ni hatari kwa usalama wa ukanda mzima.
Hayo yamesemwa na Guo Jiakun, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya "Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China, Iran, Pakistan na Russia" uliofanyika kando ya Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwamba, Tehran, Beijing, Moscow na Islamabad zinapinga jaribio lolote la kurejea kijeshi madola ya Magharibi nchini Afghanistan. Nchi hizo nne muhimu zimesema kwamba, mbali na njama hizo kuhatarisha usalama wa Afghanistan, ni tishio pia kwa amani na utulivu wa eneo hili zima.
Taarifa hiyo imesisitizia ulazima wa kuheshimiwa haki ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi yote ya Afghanistan. Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: "Wawakilishi wa nchi hizi nne wanapinga vikali kuanzishwa upya kambi za kijeshi za madola ya kigeni ndani na karibu na ardhi ya Afghanistan."
Mara kwa mara rais wa Marekani Donald Trump, amekuwa akizungumzia azma yake ya kutwaa tena udhibiti wa kambi ya jeshi la anga ya Bagram kutoka kwa Taliban. Hata tarehe 21 Septemba, Trump alitoa vitisho dhidi ya kundi la Taliban akidai kuwa mambo mabaya yataikumba Afghanistan kama hatoruhusiwa kuikalia tena kwa mabavu kambi ya Bagram. Uamuzi huo wenye utata unatokana na mambo mengi yakiwemo malengo na shabaha za kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kijiografia. Lakini muhimu zaidi ni kwamba kambi hiyo ya jeshi la anga iko kwenye eneo muhimu sana la kiistratijia.
Kambi ya Kijeshi ya Bagram iko umbali wa kilomita 40 kaskazini mwa Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. Ilijengwa na Wasovieti katika miaka ya 1950 na ilitumika kama kituo kikuu cha shughuli za kijeshi na vifaa vya Marekani na NATO nchini Afghanistan katika miaka 20 ya uvamizi wa Marekani na Wamagharibi yaani kuanzia mwaka 2001 hadi 2021. Ikiwa na barabara mbili ndefu za kurukia ndege, mabehewa makubwa ya ndege na vifaa vingi vya kilojistiki, kambi hiyo inahesabiwa kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya kijeshi nchini Afghanistan. Kambi hiyo ina uwezo mkubwa wa kupokea na kurusha droni na kusimamia kwa mbali utendaji kazi wa ndege hizo zisizo na rubani. Kambi hiyo iko karibu na mpaka wa Afghanistan na China, na suala hilo linaifanya Bagram kuwa na umuhimu usio na kifani kwa Marekani. Kituo hicho hakiko mbali sana na Iran na Russia lakini kiko karibu zaidi na China kwa umbali wa kilomita 92 tu. Trump anadai kuwa kutoka Bagram hadi kwenye vituo vya nyuklia vya China ni mwendo wa saa moja tu, hivyo lazima itekwe na ikaliwe tena kwa mabavu na Marekani.

Kwa kuongezea tu ni kwamba, huko nyuma kambi ya Bagram ilikuwa ikitumika kama kituo cha operesheni za kukabiliana na ugaidi dhidi ya vikundi kama vya al-Qaeda na ISIS. Miundombinu yake, ikiwa ni pamoja na hospitali ya vitanda 50 na gereza kubwa lenye ulinzi mkali, inasaidia kuendesha mambo kwa kina na umakini wa hali ya juu. Suhula za kambi hiyo pia zinawepesesha juhudi za kutafuta rasilimali tajiri ya madini huko Afghanistan kama vile madini ya lithiamu ambayo ni muhimu kwa mapinduzi ya teknolojia ya kisasa.
Zakir Jalali, mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Taliban, alijibu matamshi ya Trump kwa kusema kwamba Taliban kamwe hawatakubali kuwepo jeshi la kigeni nchini Afghanistan, na suala hili limekataliwa kabisa katika mazungumzo ya Doha.
Umuhimu mwingine wa kimkakati wa kambi ya kijeshi ya Bagram huko kaskazini mwa Afghanistan ni kwamba kama Marekani itaiteka na kuikalia kwa mabavu, itakuwa na uwezo wa kudhibiti taarifa za kijasusi na kiusalama katika eneo kubwa. Kupitia kuikalia tena kwa mabavu kambi ya Bagram ya Afghanistan, Marekani itaweza kufuatilia shughuli za China mashariki mwa Afghanistan, hasa karibu na mkoa wa Xinjiang, Iran upande wa magharibi na nchi za Asia ya Kati upande wa kaskazini, ambazo zinachukuliwa kuwa maeneo yenye ushawishi mkubwa wa Russia na China.
Lakini kuna jambo moja muhimu nalo ni kwamba, inaonekana Trump anajifanya kusahau uzoefu mchungu wa miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani. Nato na Marekani zilipata usoefu mchungu nchini Afghanistan na kulazimika kukimbia kwa madhila kama ilivyofanya Marekani nchini Vietnam. Vilevile uzoefu wa kihistoria wa Afghanistan unaonesha kuwa, Waafghani wanapinga vikali kukaliwa nchi yao na majeshi ya kigeni na wako tayari hata kupata hasara kubwa katika kuyatimua madola vamizi ya kigeni.