Rais wa Colombia: Trump anapasa kufungwa jela kwa jinai za Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i131464-rais_wa_colombia_trump_anapasa_kufungwa_jela_kwa_jinai_za_gaza
Rais wa Colombia, Gustavo Petro amekosoa vikali sera za mwenzake wa Marekani na kusema kuwa, Donald Trump ni mshiriki wa mauaji ya kimbari huko Gaza na anapaswa kufungwa jela.
(last modified 2025-10-01T10:49:24+00:00 )
Oct 01, 2025 10:49 UTC
  • Rais wa Colombia: Trump anapasa kufungwa jela kwa jinai za Gaza

Rais wa Colombia, Gustavo Petro amekosoa vikali sera za mwenzake wa Marekani na kusema kuwa, Donald Trump ni mshiriki wa mauaji ya kimbari huko Gaza na anapaswa kufungwa jela.

Akizungumza na waandishi wa habari, Petro amesema, "Trump hastahili chochote isipokuwa jela, kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari."

"Hakuna uharamu wowote kuhusu kutumia matokeo ya Mkataba wa Roma, iwe nchini Marekani au popote pengine," ameongeza Rais wa Petro kama alivyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.

"Ikiwa Bwana Trump ataendelea kuhusika katika mauaji ya halaiki, kama anavyofanya mpaka leo hii, hastahili chochote ila jela, na jeshi lake halipaswi kumtii," amesema Rais wa Colombia na kuongeza kuwa, "Marekani na Israel sio sehemu ya Mkataba wa Roma wa ICC, lakini Colombia ni mwanachama." 

Rais wa Colombia ameeleza bayana kuwa, "Mkataba wa Roma ndio unaofafanua uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita, na uhalifu wa kimataifa. Mtu yeyote kutoka taifa lolote anayehukumiwa na mahakama hizo anaweza kukamatwa na nchi yoyote iwapo atatia mguu katika nchi hiyo husika." 

Ikumbukwe kuwa, Septemba 27, Rais Gustavo Petro, katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alizitaka nchi za Upande wa Kusini mwa Dunia (Global South) ziunde jeshi la kimataifa ili "kuikomboa Palestina" na kukabiliana na "dhulma na ukandamizaji” unaoungwa mkono na Marekani na shirika la kijeshi la NATO.

Petro alieleza kwamba, Washington na NATO sasa hivi "zinaua demokrasia" na kufufua "uimla na ukritimba" katika upeo wa kimataifa, na akazungumzia udharura wa kuinua "bendera ya uhuru au kifo," ambayo kwa kauli yake yeye inapasa iambatane na rangi nyeupe ya amani na matumaini.