Rais Rouhani afanya mazungumzo na Marais wa Bolivia na Ecuador
(last modified Sun, 18 Sep 2016 07:13:32 GMT )
Sep 18, 2016 07:13 UTC
  • Rais Rouhani afanya mazungumzo na Marais wa Bolivia na Ecuador

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa nchi hii inakaribisha kuimarishwa uhusiano kati yake na nchi za Amerika ya Latini na khususan Bolivia katika nyanja zote.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema upo udharura kwa nchi zilizo huru kuungana na kuwa kitu kimoja ili kufanikisha malengo yao ya pamoja. Rais wa Iran aliyasema hayo jana katika mazungumzo kati yake na Rais Evo Morales wa Bolivia pambizoni mwa Kikao cha Wakuu wa Harakati ya NAM katika kisiwa cha Margarita huko Venezuela.

Rais Hassan Rouhani wa Iran akizungumza na mwenzake wa Bolivia Ivo Morales katika kisiwa cha Margarita Venezuela

Rais Rouhani amebainisha kuwa hakuna kizuizi chochote kinachokwamisha kuimarishwa ushirikiano wa pande zote kati ya Iran na Venezuela na kwamba kuimarishwa uhusiano huo ni kwa maslahi ya mataifa mawili. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa Iran iko tayari kusaidia ufanikishajii wa miradi ya maendeleo huko Bolivia na kwamba sekta binafsi katika nchi mbili hizi zinapasa kushajiishwa kwa ajili ya kuweka vitega uchumi na kushirikiana kwa pamoja. 

Kwa upande wake Rais Evo Morales wa Bolivia amemualika Rais wa Iran kushiriki kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Opec ambacho kimepangwa kufanyika mwezi Januari mwaka 2018 huko Bolivia. Rais wa Iran pia alifanya mazungumzo na Rais wa Ecuador Rafael Correa Delgado na kuashiria masuala yanayoziunganisha pamoja nchi mbili hizo na kueleza kuwa, Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na Ecuador katika nyanja zote.