Unicef yatahadharisha kuhusu utapiamlo kwa watoto
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limetahadharisha kuhusu utapiamlo unaowasibu watoto katika nchi zinazoendelea duniani.
Unicef imetahadharisha katika ripoti iliyotoa hii leo kuhusu utapiamlo unaowasumbua watoto katika nchi zinazoendelea na kueleza kuwa, kati ya watoto sita walio na umri chini ya miaka miwili katika nchi zinazostawi, watato watano hawapati lishe iliyo salama na ya kutosha; jambo linawafanya watoto hao wawe katika hatari ya kupatwa na matatizo ya kiakili na kimwili.
Ripoti ya shirika la Unicef imeongeza kuwa, theluthi moja ya watoto katika nchi zinazoendelea huwa hawapati lishe salama katika miezi sita ya awali ya maisha yao. Ripoti hiyo imeendelea kubainisha kuwa, ubora na kiwango cha chakula kinachotakikana kwa ajili ya afya na makuzi ya watoto kinaweza kuokoa maisha ya watoto laki moja kila mwaka na kupunguza pia gharama za matibabu kwa kundi hilo tajwa.
Huko nyuma Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa liliripoti kuwa, watoto karibu milioni 385 wanaishi katika familia ambazo pato lake la siku ni la kiwango cha chini sana, huku nusu ya watoto hao maskini wakiishi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, na wengine zaidi ya theluthi moja wakiishi kusini mwa bara la Asia.