Magaidi washambulia chuo cha polisi na kuua 55 nchini Pakistan
Makumi ya makurutu wameuawa baada ya genge la kigaidi kushambulia chuo cha kutoa mafunzo ya polisi kusini magharibi mwa Pakistan.
Katika hujuma hiyo ya usiku wa kuamkia leo katika mji wa Quetta mkoani Balochestan, magaidi watano walishambulia kwa risasi taasisi hiyo ya makurutu wa polisi na kuua 55 miongoni mwako mbali na kujeruhi wengine zaidi ya 100.
Sarfaraz Bugti, Waziri wa Mambo ya Ndani wa mkoa huo amethibitisha kutokea hujuma hiyo ya kigaidi na kuongeza kuwa, magaidi hao walianza kufyatua risasi ovyo baada ya kuingia chuoni hapo na kuwaua walinzi na kisha kuwashika mateka baadhi ya makurutu hao.
Itakumbukwa kuwa, Septemba 16, watu wasiopungua 23 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanywa ndani ya msikiti katika Sala ya Ijumaa wilayani Mohmand nchini Pakistan.
Mnamo mwezi Juni 2014, jeshi la Pakistan lilianzisha operesheni ya kuyatokomeza makundi yanayobeba silaha katika maeneo ya kikabila huko kaskazini magharibi mwa nchi kwa lengo la kuhitimisha wimbi la machafuko lililoanza mwaka 2004 na kusababisha vifo vya maelfu ya raia.
Hali ya usalama imeboreka nchini Pakistan katika miaka ya karibuni, ambapo kwa mujibu wa jeshi, idadi ya "matukio ya kigaidi" imepungua kutoka 128 mwaka 2013 hadi 74 mwaka uliopita wa 2015, japokuwa mashambulio makubwa katika maeneo yaliyo rahisi kushambuliwa yangali yanaendelea kushuhudiwa.