Trump: Ni lazima niibuke mshindi Marekani, vyombo vya habari acheni uongo
Mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa rais nchini Marekani amesema kuwa, ni lazima ataibuka mshindi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika siku chache zijazo, huku akivituhumu vyombo vya habari vya Marekani kuwa vinamuunga mkono hasimu wake na kupotosha ukweli.
Donald Trump ameyasema hayo kufuatia matokeo ya hivi karibuni ya uchunguzi wa maoni nchini Marekani na kusema kuwa, lazima niwe mshindi katika uchaguzi huo. Akiwahutubia wafuasi wake katika jimbo la Ohio, Trump amesisitiza kuwa, sasa ni wakati wa kuibuka washindi wanachama wa chama cha Republican na kutwaa ikulu ya Marekani 'White House' kutoka mikononi mwa Wademokrat.
Trump amevituhumu vyombo vya habari kuwa vinamuunga mkono hasimu wake Hillary Clinton, na kusema kuwa mwenendo huo haufai. Ameenda mbali na kusema kwamba, hata katika majimbo ya Carolina Kaskazini, Iowa, Ohio na Florida ambayo uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Hillary Clinton ataongoza kwa kura, pia ni yeye atakayeibuka mshindi na si vinginevyo. Kadhalika amesema kuwa Hillary Clinton ni mwongo mkubwa na amewataka Wamarekani kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo kwa maslahi yake. Uchaguzi wa rais nchini Marekani umepangwa kufanyika tarehe 8 Novemba mwaka huu, na kila jimbo litapiga kura kwa kujitegema.