Maulama wa Yemen wakadhibisha madai ya Saudia, miji mitakatifu haishambuliwi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i18787-maulama_wa_yemen_wakadhibisha_madai_ya_saudia_miji_mitakatifu_haishambuliwi
Maulama wa Kiislamu nchini Yemen wamekadhibisha madai yaliyotolewa na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia uliosema jeshi na wapiganaji wa Yemen wameshambulia mji mtakatifu wa Makka.
(last modified 2025-10-23T09:42:35+00:00 )
Nov 04, 2016 08:16 UTC
  • Maulama wa Yemen wakadhibisha madai ya Saudia, miji mitakatifu haishambuliwi

Maulama wa Kiislamu nchini Yemen wamekadhibisha madai yaliyotolewa na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia uliosema jeshi na wapiganaji wa Yemen wameshambulia mji mtakatifu wa Makka.

Taarifa iliyotolewa na mkutano uliojumuisha maulama na wanazuoni wa madhehebu mbalimbali mjini San'aa imesema utawala wa Saudi Arabia unatumia Haramu Mbili tukufu za Makka na Madina kwa ajili ya malengo yake ya kikoloni na kwamba madai yasiyo ya kweli kwamba jeshi na makundi ya wapiganaji wa Yemen yameshambulia ardhi tukufu ya Makka ni uongo ambao hautawahadaa waumini wala kufunika jinai na mauaji ya kinyama yanayoendelea kufanywa na utawala huo ukishirikiana na Marekani dhidi ya watu wa Yemen.

Taarifa ya wanazuoni wa Kiislamu wa Yemen imesema: Madai na propaganda za vyombo vya habari vya Saudia kwamba wapiganaji wa Yemen wameshambulia mji wa Makka ni hadaa inayokusudiwa kuficha jinai za Saudia na Marekani na imewataka wasomi na Waislamu kwa ujumla kutohadaiwa na hila hizo.

Vilevile wanazuoni wa madhehebu za Kiislamu nchini Yemen wamepongeza juhudi kubwa za jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi hususan Kikosi cha Makombora kwa mafanikio yao makubwa na kulitaka taifa la Yemen kuendelea kusimama kidete katika kukabiliana na uadui wa Saudia na washirika wake.

Kombora la Burkan-1

Inafaa kukumbusha kuwa, siku chache zilizopita wanamapambano wa Yemen walijibu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo kwa kuvurumisha makombora ya Burkan-1 na kupiga uwanja wa ndege wa Mfalme Abdul Aziz katika mji wa Jiddah. Hii ni mara ya kwanza kwa Kikosi cha Makombora cha Yemen kulenga na kuupiga kwa makombora mji wa Jiddah ambao ni makao makuu ya kiuchumi ya Saudi Arabia. Baada ya mafanikio hayo ya aina yake utawala wa kifalme wa Aal Saud ulieneza propaganda na uongo kupitia vyombo vya habari ukidai kuwa mashambulizi hayo yaliulenga mji mtukufu wa Makka.

Burkan-1

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, tarehe 10 mwezi wa Oktoba Kikosi cha Makombora cha Yemen pia kilishambulia kituo cha jeshi la anga la Saudia cha Mfalme Fahad kwa kutumia makombora hayo hayo ya Burkan-1 yenye uwezo wa kulenga shabaha zaidi ya umbali wa kilomita 800.