Zarif amuonya Trump asithubutu kukiuka mapatano ya nyuklia ya Iran
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif ameonya kuwa iwapo rais mteule wa Marekani atakiuka mapatano ya nyuklia, basi Iran ina machaguo mengine ya kukabiliana na hali hiyo.
Akizungumza mjini Prague siku ya Ijumaa akiwa ameandamana na mwenzake wa Jamhuri ya Czech Lumbomir Zoralek, Zarif amesisitiza kuwa Iran inafungamana kikamilifu na utekeelzaji wa mapatano ya nyuklia baina yake na madola sita makubwa duniani yaliyotiwa saini mwaka jana. Aidha ameikosoa Marekani kwa kutotokeleza kikamilifu majukumu yake katika mapatano hayo ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Utekelezwaji, JCPOA.
Iran na nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia Julai 14 mwaka jana na kuanza kuyatekeleza Januari 16 mwaka huu. Zarif amesema pande mbili zilifanya mazungumzo ya miezi 23 mfululizo kabla ya kufikia mwafaka. Akizungumza Jumatano baada ya ushindi wa Donald Trump kama rais wa Marekani, Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema mapatano ya JCPOA ni 'azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa' na hayawezi kubadilika kwa uamuzi wa serikali moja.
Rais mteule wa Marekani Trump aliwahi kusema wakati wa kampeni kuwa, mapatano ya nyuklia ya Iran ni 'maafa' na kwamba ni 'mapatano mabaya zaidi duniani'. Aliahidi kuyatupilia mbali katika siku yake ya kwanza katika Ikulu ya White House na kusema ni lazima Iran iendelee kuwekewa vikwazo.
Pamoja na hayo, Walid Phares mshauri wa Trump katika sera za kigeni akizungumza baada ya ushindi wake katika uchaguzi amesema kunapaswa kufanyika mazungumzo ya kutathmini upya mapatano ya nyuklia ya Iran.