ICC yakiri kuwa Marekani ilitenda jinai za kivita Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19501-icc_yakiri_kuwa_marekani_ilitenda_jinai_za_kivita_afghanistan
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imesema wanajeshi wa Marekani na maafisa wa shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA yumkini wana hatia ya kufanya jinai dhidi ya binadamu nchini Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 15, 2016 04:28 UTC
  • ICC yakiri kuwa Marekani ilitenda jinai za kivita Afghanistan

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imesema wanajeshi wa Marekani na maafisa wa shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA yumkini wana hatia ya kufanya jinai dhidi ya binadamu nchini Afghanistan.

Akizungumza hapo jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya awali kuhusu jinai za Marekani nchini Afghanistan, Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC amesema kuna msingi wenye mantiki wa kuamini kuwa, wanajeshi wa Marekani pamoja na maafisa wa CIA walitenda jinai za kivita dhidi ya 'wafungwa' wa Afghanistan kati ya mwaka 2003 na 2004. Bensouda amebainisha kuwa, maafisa hao wa Marekani waliwatesa, kuwabaka na kuwadhalilisha washukiwa wa ugaidi ikiwa ni katika mbinu zao za 'kutafuta taarifa za kiintelijensia' kutoka kwao.

Askari wa Marekani nchini Afghanistan

Licha ya ripoti hiyo ya ICC, lakini Marekani hadi sasa inaendelea kutenda jinai za kutisha dhidi ya raia wa Afghanistan. Novemba 2, watu 30 waliuawa katika shambulio la anga lililofanywa na ndege za Marekani katika mkoa wa Kunduz, kaskazini mwa nchi hiyo. Kadhalika Novemba mwaka jana, Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ilithibitisha kuwa raia zaidi ya 40 waliuawa katika shambulio lililofanywa na ndege za kivita za Marekani dhidi ya hospitali ya jumuiya hiyo katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan mnamo Oktoba 3 mwaka jana.

Shambulizi la Septemba 11 nchini Marekani, linalodaiwa kufanywa na Taliban

Marekani iliivamia Afghanistan mwaka 2001, kwa kile Washington ilidai kuwa 'ni vita dhidi ya ugaidi', kufuatia shambulizi la Septemba 11 nchini Marekani.