Nov 25, 2016 06:56 UTC
  • HRW yamtaka rais mteule wa Marekani kuheshimu sheria za kibinadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limemtaka rais mteule wa Marekani kuheshimu sheria za kimataifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch, Kenneth Roth amemtaka Donald Trump kutupilia mbali mipango yake iliyozusha makelele na mjadala mkubwa katika kipindi cha kampeni za uchagzi wa rais wa Marekani na kuheshimu sheria za kimataifa.

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais, Donald Trump alitoa matamshi yaliyozusha mjadala mkubwa dhidi ya Waislamu, wahajiri na makundi mengine ya waliowachache katika jamii ya Marekani ambayo yalikosolewa sana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump

Rais mteule wa Marekani pia ametoa wito wa kuanzishwa kituo cha upelelezi cha kufuatilia nyendo za wafuasi wa dini ya Uislamu nchini humo na kusisitiza kuwa hapana budi kufungwa misikiti na maeneo ya ibada ya Waislamu.

Miongoni mwa misimamo ya Donald Trump iliyozusha mjadala mkubwa ni kuhusu mpango wake wa kujenga ukuta wa kuzuia wahajiri wa kimexico kuingia nchini Marekani katika mpaka wa nchi hizo mbili, kufuta bima ya afya maarufu kama Obamacare na kufutwa au kurekebisha mikataba ya biashara huru.   

Tags