UN yatiwa wasiwasi na kuongezeka machafuko Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umesema kuwa una wasiwasi na kushtadi machafuko ya kikabila huko Sudan Kusini.
Yasmin Sooka Mkuu wa Kundi la Wataalamu wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ambaye ameelekea Sudan Kusini alisema jana akiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba kuwa machafuko na ghasia za kikabila zinashuhudiwa katika maeneo yote ya Sudan Kusini.
Yasmin Sooka amesisitiza kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini, na kutaka kutumwa nchini humo wanajeshi wengine wa kudumisha amani wapatao 4000. Mkuu huyo wa Kundi la Wataalamu wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ametaka pia kuundwa mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za jinai za kivita huko Sudan Kusini. Sudan Kusini ambayo ilipata uhuru wake mwaka 2011, imeathiriwa na vita vya ndani tangu mwezi Disemba mwaka 2013; vita ambavyo vimesababisha kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kupelekea wengine milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi.