Dec 01, 2016 15:01 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN ataka watu wenye Ukimwi wasaidiwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusaidiwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Ban Ki-moon ambaye alikuwa akizungumza kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ukimwi amesisitiza haja ya kuacha unyanyapaa na unyanyasaji dhidi ya wale wanaoishi na ugonjwa huo na kuhakikisha kuwa, wanapata huduma, matibabu na ulinzi wanaostahiki.

Ban ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kushughulikia ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kupunguza nusu ya idadi ya watoto wanaoambukizwa virusi vya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuzidishwa mara dufu idadi ya watu wanaopata madawa ya kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Ban Ki-moon akiwa na mwathirika Mkenya, Rebecca Awiti na watoto wake watatu 

Vilevile ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kuhakikisha kwamba, lengo la kutoa tiba kwa watu milioni 30 ifikapo mwaka 2030 linatimizwa kwa kutoa huduma kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatarishi, wanawake vijana wa maeneo ya kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika na watu maskini wanaohitaji huduma na tiba.  

Wakati huo huo Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema kuna haja ya kuongezwa vifaa vya kupimia virusi hivyo hatari majumbani ikizingatiwa kuwa watu wengi wanaogopa kwenda kupimwa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya vya umma.

Margaret Chan

Chan amesema kuwa, asilimia 40 ya watu wenye virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi, sawa na watu milioni 14 kote duniani, hawajafanyiwa vipimo kutambua hali zao za kiafya.

Siku ya Kimataifa ya Ukimwi huadhimishwa kila mwaka tarehe Mosi Disemba. 

Tags