Nov 30, 2022 10:58 UTC
  • Waziri: Ukimwi unaua Waganda 46 kila siku

Waziri katika Ofisi ya Rais nchini Uganda ameashiria ongezeko la maambukizi ya virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi miongoni mwa tabaka la vijana wanaobaleghe nchini humo na kusema kuwa, maradhi hayo yanaua Waganda 46 kwa siku.

Milly Babalanda amesema hayo akinukuu takwimu za Wizara ya Afya ya Uganda zinazoonesha kuwa, asilimia 37 ya kesi mpya za mambukizi ya HIV zilizorekodiwa mwaka jana, zilikuwa miongoni mwa vijana wenye miaka 15-24.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, watu 1,000 nchini Uganda wanaambukizwa HIV kila wiki, huku vifo 325 vinavyohusishwa na maradhi ya Ukimwi katika kipindi hicho cha siku saba.

Takwimu za Wizara ya Afya ya Uganda zinaonesha kuwa, Waganda milioni 1.4 wanaishi na virusi vya HIV katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya kuwa, huenda watu milioni moja wenye virusi vya HIV na wanaougua maradhi ya Kifua Kikuu (TB) wakapoteza maisha kutokana na janga la corona kuwasimamishia matibabu.

Kwa mujibu wa WHO, janga la corona limekuwa na taathira hasi kwa sekta ya afya duniani, kutokana na kuvuruga utoaji wa matibabu kwa wenye magonjwa mbalimabali.

Haya yanajiri huku Uganda ikijiandaa kuungana na ulimwengu katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo huadhimishwa Disemba Mosi kila mwaka.

 

Tags