Jul 15, 2021 07:47 UTC
  • Wenye UKIMWI hatarini maradufu kufa kwa Corona

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI inaonyesha kuwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi au VVU wako katika hatari zaidi ya kuugua ugonjwa wa Corona au COVID-19 na hata kufariki dunia lakini bado wananyimwa haki ya kupata chanjo dhidi ya Corona.

Ripoti hiyo imetolewa Geneva, Uswisi na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS kwa anuani ya ripoti ya Kukabiliana na Ukosefu wa Usawa mwaka 2021 na ina ushahidi dhahiri kuwa ukosefu wa usawa unawafanya watu hao wanaoishi na VVU washindwe kupata chanjo dhidi ya COVID-19 na VVU.

Tafiti zilizofanyika Uingereza na Afrika Kusini zimeonyesha kuwa hatari ya mtu anayeishi na VVU kufariki dunia kwa COVID-19 ni maradufu zaidi ya mtu asiye na VVU.

Katika nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa jangwa la Sahara ambako kuna asilimia 67 ya watu wote wanaoishi na VVU duniani kote, ni chini ya asilimia 3 ya watu hao ndio wamepata angalau dozi ya kwanza ya COVID-19 hadi mwezi huu wa Julai.

Wakati huo huo, huduma za kinga dhidi ya VVU pamoja na matibabu zinaengua makundi muhimu na watoto na barubaru.

Ripoti hiyo inasema chanjo dhidi ya COVID-19 zinaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea, “lakini zinahodhiwa na nchi tajiri na mashirika katika uzalishaji na usambazaji kwa lengo la kujipatia faida. Hii ina madhara makubwa katika mfumo wa afya kwenye nchi zinazoendelea kwani mifumo hiyo imezidiwa uwezo. Mfano Uganda, ambako viwanja vya mpira wa miguu vimegeuzwa kuwa hospitali za muda.”

Akizungumzia hali hiyo ya utata na sutafahamu kuhusu pengo la utoaji chanjo kati ya nchi tajiri na zile maskini, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima amesema, “nchi tajiri barani Ulaya zinajiandaa kufurahia majira ya kiangazi kwa kuwa wananchi wao wamepata chanjo dhidi ya COVID-19 ilhali nchi maskini ziko katika janga”Bi. Byanyima amesema dunia imeshindwa kupata somo kutokana na VVU wakati mamilioni ya watu walioponyimwa dawa muhimu za kuokoa maisha yao, walikufa kwa sababu ya ukosefu wa usawa. “Hii haikubaliki”, amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNAIDS.../

 

Tags