Mkutano wa Umoja wa Kiislamu wafanyika Ivory Coast
Mkutano wa kwanza wa Umoja wa Kiislamu umefanyika nchini Ivory Coast ukiwashirikisha wahadhiri wa vyuo vikuu, wanachuo na wanafunzi wa shule za Kiislamu nchini humo mjini Abidjan.
Mkutano huo umesimamiwa na ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al Mustafa cha Qum nchini Iran. Wazungumzaji katika mkutano huo wa Umoja wa Kiislamu wametilia mkazo mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani na Hadithi na udharura wa kulindwa umoja na mshikamano baina ya makundi mbalimbali ya Waislamu.
Mwanzoni mwa mkutano, huo balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ivory Coast, Mansour Shekib Mehr amesoma sehemu ya ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei unaosisitiza umuhimu wa Waislamu kushikamana na kujiepusha na hitilafu na uhasama na kusema kuwa, Iran ya Kiislamu daima imekuwa ikihubiri mshikamano na umoja kati ya Waislamu wote.

Mjumbe wa timu ya Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu, Muhammad Hussein Wasiti ambaye pia amehutubia mkutano huo amewahimiza maulama na wanazuoni wa Kiislamu kufasiri na kubainisha vyema mafundisho ya Uislamu ili kuzuia baadhi ya watu kuzusha hitilafu na migawanyiko kutokana na ufahamu usio sahihi wa mafundisho ya dini hiyo.
Kwa upande wake Sheikh Sharif Umar Abdul Aziz ambaye ni miongoni mwa wanafikra wa Ivory Coast amesema kuwa umoja na mshikamano wa Kiislamu ndiyo njia pekee ya kufika kwa Mwenyezi Mungu na amesisitiza udharura wa kuheshimiana kama msingi wa umoja na mshikamano.

Waislamu nchini Ivory Coast wanaunda asilimia 39, Wakristo 33 na asilimia iliyobaki inaundwa na wafusi wa dini na madhehebu nyingine.