UN yataka Suu Kyi azuie mauaji ya Waislamu Myanmar
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa kiongozi asiye rasmi wa Myanmar Aung San Suu Kyi achukue hatua za kuzuia ukatili wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika taarifa, mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Vijay Nambiar, ametoa wito moja kwa moja kwa Suu Kyi kuingilia na kusitisha jinai za jeshi dhidi ya Waislamu.
Aidha amemtaka Suu Kyi binafsi kutembelea jimbo la Rakhine ili Waislamu wapate hakikisho kuwa hawataendelea kuteswa.
Suu Kyi ambaye anapigiwa debe na nchi za Magharibi kuwa eti ni 'nembo ya demokrasia' amelaumiwa vikali kwa kutochukua hatua yoyote ya maana kuwalinda Waislamu wa Rohingya ambao mashirika ya haki za binadamu yanasema wanaangamizwa kwa umati na jeshi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.