UNICEF yatahadharisha kuhusu hali ya maisha ya watoto duniani
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa watoto wapatao milioni 535, ambao ni sawa na robo moja ya watoto wote duniani wanaishi kwenye nchi zenye migogoro au zinazokabiliwa na maafa ya kimaumbile.
UNICEF imeeleza kupitia taarifa kuwa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika takribani robo tatu ya watoto wanaishi katika nchi zenye mazingira hatarishi wakishindwa kupata huduma za afya, elimu bora, lishe inayoridhisha na matunzo yanayostahiki.
Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa sambamba na kukaribia maadhimisho ya mwaka wa 70 tangu kuasisiwa Mfuko huo wa Umoja wa Mataifa wa kuhudumia watoto, hali hiyo inaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika ambako inaishi asilimia 12 ya watoto wote duniani.
UNICEF imebainisha katika taarifa yake kuwa kutokana na migogoro, maafa ya kimaumbile na mabadiliko ya tabianchi, watoto hulazimika kutoroka makwao au kuangukia kwenye medani za vita na kukabiliwa na hatari ya kupatwa na maradhi, kufanyiwa ukatili na hata kutumiwa vibaya. Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, hali ya hatari ambayo watoto wenye hali mbaya wanakabiliana nayo leo hii, inatishia hatua za kuridhisha zilizopigwa katika miaka ya karibuni…/