Maandamano makubwa ya kuwaunga mkono wahajiri yafanyika Uhispania
Katika hali ambayo Rais Donald Trump wa Marekani anatazamiwa wiki ijayo kutangaza 'sheria kali zaidi' za kudhibiti wahajiri na raia wa nchi saba za Kiislamu, mamia ya maelfu ya wananchi wamefanya maandamano Uhispania kuonyesha uungaji mkono wao kwa wajahiri.
Maandamano hayo ya jana Jumapili mjini Barcelona yaliyoandaliwa na vuguvugu linaloitwa Casa Nostra Casa Vostra (Kwetu ni Kwenu), yalivutia idadi kubwa ya watu, shakhsia na wanaharakati mbali mbali wa kutetea haki za binadamu wa Uhipania. Kundi hilo lililoandaa maandamano hayo linasema zaidi ya watu laki tatu walishiriki maandamano hayo ingawaje duru za polisi zinasema ni watu laki moja na 60 elfu ndio walioshiriki.
Baadhi ya jumbe zilizokuwa kwenye mabango yaliyobebwa na waandamanaji hao zilisema "Hakuna vijisababu, Wapokee Wote" na "Fungueni mipaka, hatutaki maafa zaidi".
Ada Colau, Meya wa mji wa Barcelona ambaye alishikiri maandamano hayo amesema kuwa, Barcelona utakuwa mji wa matumaini, kwa kuwa takriban maeneo mengine yote ya bara Ulaya yamegeuka na kuwa chimbuko la chuki dhidi ya wageni na wahajiri.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri OIM, zaidi ya wahajiri elfu tano walifariki dunia tangu mwezi Aprili mwaka jana hadi Disemba, kwa kuzama baharini wakijaribu kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, huku mamia ya maelfu ya wengine wakirejeshwa makwao baada ya kuwasili katika baadhi ya nchi za bara hilo.