Daesh laua zaidi ya watu 30 katika hospitali ya kijeshi Afghanistan
Wanamgambo waliojizatiti kwa silaha nzito wameua zaidi ya watu 30 na kuwajeruhi wengine wapatao 50 katika shambulio walilofanya dhidi ya hospitali kubwa zaidi ya kijeshi ya Sardar Daud Khan iliyopo katikati mwa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan Dawlat Waziri amesema shambulio hilo lilianza majira ya tatu asubuhi ya leo kwa mripuko mkubwa uliotokea kwenye lango la mbele la kuingilia hospitalini hapo. Washambuliaji waliovamia hospitali hiyo walikuwa wamevalia sare za madaktari huku wakiwa wamebeba bunduki za rashasha na mabomu ya mkono.
Dawlat Waziri ameongeza kuwa washambuliaji hao wanne nao pia waliuliwa wakati wa shambulio hilo dhidi ya hospitali hiyo iliyoko kwenye eneo la majengo ya kidiplomasia yanayopewa ulinzi mkali ukiwemo ubalozi wa Marekani.
Vyombo vya habari vimemnukuu Waziri akisema akthari ya waliouliwa na kujeruhiwa ni wagonjwa, madaktari na wauguzi.
Mmoja wa wauguzi kwa jina la Abdul Qadeer, amesema: "Nilimwona mmoja wa washambuliaji akiwa na bunduki aina ya AK-47 akiwa amevalia sare ya daktari akiwafyatulia risasi wagonjwa na walinzi katika ghorofa ya tatu".
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na shambulio hilo ambalo liliendelea kwa muda wa saa sita na kuzusha mtafaruku ndani ya hospitali hiyo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Bahram Qassemi imelaani shambulio hilo. Qassemi amesisitiza kuwa njia pekee ya kupambana na baa la ugaidi nchini Afghanistan na katika eneo ni kuwepo mwafaka wa pamoja kimataifa wa kuzuia mianya na njia za kupitishia misaada ya kimaanawi na kimaada kwa makundi ya kigaidi.../