Mafuriko, maporomoko ya udongo yaua 250 nchini Colombia
Kwa akali watu 254 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo katika mkoa wa Putumayo kusini mwa Colombia.
Rais wa Colombia Juan Manuel Santos amethibitisha kutokea janga hilo na kuongeza kuwa, mbali na watu 400 kujeruhiwa, makumi ya maelfu ya wengine wamelazimika kuyahama makazi hayo kutokana na mafuriko hayo, yaliyotokea baada ya mto mmoja kuvunja kingo zake katika mji wa Mocoa, kusini mwa nchi.
Carlos Ivan Marquez, Afisa wa Shirika la Kukabili Majanga nchini humo amesema kuwa, yumkini idadi ya waliofariki dunia kutokana na janga hilo ikaongezeka, kwa kuwa hadi sasa hawajui hatima ya mamia ya watu waliotoweka na waliofukiwa katika vifusi vya nyumba zao katika eneo hilo.
Meya wa mji wa Mocoa, Jose Antonio Castro amesema shughuli zimekwama kikamilifu katika mji huo kutokana na janga hilo, haswa kwa kuzingatia kuwa barabara zimefungwa na mawasiliano kukatika.
Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 20 elfu walipoteza maisha katika maporomoko mengine ya ardhi yaliyotokea nchini Colombia mwaka 1985 katika eneo la Armero.