Jumuiya ya Wafanyakazi Norway yataka kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina
Jumuiya ya Wafanyakazi nchini Norway imetoa wito wa katambulwia rasmi nchi huru ya Palestina.
Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Wafanyakazi nchini Norway imetoa wito wa kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina na kuwekwa vikwazo vya biashara dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Shaawan Jabbarin, Mkurugenzi wa Taasisi ya Haqq inayotetea haki za taifa la Palestina huko Norway pia ametoa wito wa kuvunjwa mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kususiwa bidhaa zote zinazotengenezwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina.
Jabbarin ametahadahrisha kuwa, serikali ya Norway itakuwa imekiuka sheria za kimataifa iwapo itashiriki katika mkataba wa kuchimba mafuta na gesi katika maeneo ya Bahari ya Mediterania yanayotambuliwa na jamii ya kimataifa kuwa yanakaliwa kwa mabavu.
Nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa zimekuwa zikitoa wito wa kususiwa Israel kutokana na jinai zinaoendelea kufanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina.
Miezi kadhaa iliyopita Mji mkuu wa Iceland ulitangaza kuwa wakazi wake wamepiga kura ya kuunga mkono kususiwa bidhaa zinazozalishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel hadi pale Palestina itakapotangazwa kuwa taifa huru.